Sudan haijateteleka kuhusu suala la Darfur. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sudan haijateteleka kuhusu suala la Darfur.

Serikali ya Sudan haitarajiwi hivi karibuni kuregeza msimamo wake kuhusu kupelekwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika eneo la Darfur, hata ingawa afisa mmoja mkuu wa Marekani amepangiwa kuitembelea nchi hiyo baadaye juma hili. Hata hivyo, kuna chembe ya matumaini ya kuongezwa msaada wa hali na mali kwa Kikosi cha Umoja wa Afrika kinachotoa huduma katika eneo hilo linalokabiliwa na mzozo.

Mwanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Afrika akishika doria katika eneo la Darfur

Mwanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Afrika akishika doria katika eneo la Darfur

Waziri msaidizi wa mambo ya nje wa Marekani, John Negroponte, anatarajiwa kuwasilisha ujumbe mkali kwa serikali ya Sudan kuhusu eneo la Darfur.

Marekani imetishia kuachukua hatua nyingine mpya kuishinikiza Sudan kuruhusu kupelekwa kikosi cha Umoja wa Mataifa kusaidia majeshi ya Umoja wa Afrika yanayokabiliwa na uhaba wa vitendea kazi.

Umoja wa Afrika una kiasi wanajeshi elfu saba katika Darfur.

Ghasia zimekuwa zikiendelea katika eneo hilo hata baada ya serikali kutia saini mwafaka wa amani mwaka uliopita kati yake na kundi moja la waasi.

Mapema mwezi huu wapiganaji wa eneo hilo ambao hawakujulikana waliwaua wanajeshi watano wa Umoja wa Afrika.

John Negroponte anatarajiwa pia kuzitembelea Chad na Libya ambazo zinahusika kwa namna fulani kwenye mzozo huo.

Hata hivyo haijafahamika kinaga ubaga wakati ambao waziri msaidizi huyo wa Marekani atawasili nchini Sudan.

Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye ameondokea kuwa maarufu kwa kupatanisha makundi hasimu barani Afrika, atawasili Sudan leo na anatarajiwa kulizungumzia tatizo la Darfur.

Matokeo ya mkutano uliofanyika, Addis Ababa mwezi Novemba mwaka jana, yamegubika suala hilo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Sudan ilikubali wakati wa mkutano huo mpango wa awamu tatu ambao ungemalizikia kwa kuundwa kikosi cha pamoja kilichojumuisha vikosi vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Sudan nayo inadai kwamba iliridhia awamu mbili za mwanzo za mpango huo ambazo zililenga kutoa msaada wa hali na mali.

Siku ya Jumamosi iliyopita, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Alpha Oumar Konare aliunga mkono msimamo wa Sudan aliposhauriana na Rais Omar Hassan al-Bashir.

Alpha Oumar Konare alisema mkutano wa Addis Ababa ulitoa mapendekezo ya wazi kuhusu kuundwa kwa kikosi hicho ambacho kingepata ufadhili wa hali na mali kutoka Umoja wa Mataifa.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika alisema hapajakuweko makubaliano kuhusu idadi inayohitajika ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika.

Wakuu wa Umoja wa Mataifa na wale wa Umoja wa Afrika jana walikuwa kwenye kikao cha kiufundi mjini Addis Ababa kulishughulikia suala hilo.

Maafisa wa Marekani wamearifu wako karibu kuanzisha hatua mpya dhidi ya Sudan, lakini harakati yao inaonekana kucheleweshwa kidogo hususan baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kusema anahitaji muda zaidi wa kuibembeleza Sudan kukubali kikosi hicho cha pamoja.

Miongoni mwa hatua ambazo Marekani inapanga kuchukua ni kuongeza idadi ya makampuni kwenye orodha ya makampuni yasiyoruhusiwa kufanya biashara nchini Sudan, kukataza makampuni ya Sudan kutumia dola kwenye bishara zao na pia kupiga marufuku ya kusafiri dhidi ya wakuu kiasi watatu wa Sudan.

Marekani pia inapanga kulifadhili kundi la SPLA kijeshi kwa lengo la kuyatatiza majeshi ya Sudan.

Sudan haijateteleka hata chembe! Kwanza haijapata shinikizo kutoka Umoja wa Afrika na pia inaungwa mkono na China.

Wataalamu wanakadiria watu laki mbili wameuawa na wengine milioni mbili na nusu wamekimbia makazi yao katika eneo la Darfur tangu mzozo huo ulipoanza mwaka 2003.

Serikali ya Sudan inasema watu elfu tisa pekee ndio waliofariki mpaka sasa.

Siku ya jumamosi iliyopita, serikali hiyo iliyashutumu mataifa ya Ulaya kwa kukosa kukisaidia kikosi cha Afrika ili yapate kisingizio cha kupendekeza kikosi cha Umoja wa Mataifa kipelekwe katika eneo la Darfur.
 • Tarehe 09.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGi
 • Tarehe 09.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGi

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com