Stuttgart yaizaba Bremen 6:3 | Michezo | DW | 10.03.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Stuttgart yaizaba Bremen 6:3

Katika bundesliga-B.Munich yapanua mwanya wake hadi pointi 7 kileleni baada ya stuttgart kuitandika Bremen 6:3.

default

Mario Gomez wa Stuttgart

Katika Bundesliga-Bayern Munich imepanua mwanya wake kutoka Werder Bremen kwa pointi 7 baada ya bremen kukomewa mabao 6-3 na stuttgart hapo jumamosi.

Mwanariadha wa ethiopia –bingwa wa olimpik wa masafa ya mita 5000 Meseret defar ashinda mbio za mita 3000 mjini Stuttgart kusini mwa Ujerumani wakati Mnigeria Samuel Peter amedengua mrusi Oleg Maskaev katika duru ya 6 huko Cancumn,Mexico na kuvaa taji la WBC la wezani wa juu ulimwenguni.

Tukianza na Bundesliga-viongozi wa Ligi-Bayern Munich wazidi kutanua mwanya wao kileleni mwa Bundesliga baada ya jumamosi kutamba nyumbani allianz Arena mbele ya Karlsruhe SC na kuwachapa mabao 2:0.

Mahasimu wao wakubwa katika kinyan’ganyiro cha taji la ubingwa Werder Bremen waliteleza vibaya sana jumamosi walipowatembelea mabingwa stuttgart.

Bremen ilikandikwa mabao 6-3 na Stuttgart na hivyo iko nyuma sasa kwa pointi 7 kutoka kileleni.Hamburg jana iliweza kuipiga kumbo Bremen kutoka nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi ingawa hamburg ilimudu sare tu ya 0:0 na Nüremberg.

Hii haikumridhisha kocha wa Hamburg Huub Stevens alietaka jana kuondoka na pointi zote 3 badala ya sare.Alisema,

“Hatuna kikosi kikubwa kama kile cha Bayern Munich na hili nilikwishasema tangu mwanzo .Na ikiwa wachezaji 6 si fit kucheza hii huwa na athari zake katika timu.”

Alinungunika mholanzi huyo kocha wa Hamburg ilioangukia sasa nafasi ya 3 ya ngazi ya Ligi nyuma ya Bayern Munich.

Schalke iliokata tiketi ya robo-finali ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya kati ya wiki iliopita ,iliilaza Armenia Bielefeld mabao 2-0 na sasa imeangukia nafasi ya 5 ya ngazi ya Ligi.Katika zahama ya timu mbili ziliopo mkiani mwa Bundesliga Hansa Rostock na Duisburg,timu hizo 2 ziliachana sare bao 1:1.

Bayer Leverkusen iliitandika Hannover 96 mabao 2:0.

Akionekana ameridhishwa na matokeo hayo, kocha wa Leverkusen Michael Skibbe alisema:

“Mbali na mkwaju wa kutuonya langoni mwetu katika kipindi cha kwsanza ,sisi tuliudhibiti mcehzo kwa muda wa kipindi kizima cha dakika 90.”

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la FA nchini Uingereza,mshammbulizi wa Chelsea Nicholas Aneilka alisema wachezaji wachezaji wapaswa kujitwikalawama kwa kudhalilishwa hapo jumamosi na Barnsley na sio kocha Avram Grant.

Kocha huyo wa kiisraeli aliungama kwamba anakodolewa sasa macho makali kwa mara nyengine tena baada ya Chelsea kulazwa katika robo-finali ya kombe hilo la FA huko Yorkshire.Pigo hilo linafuatia karibu sana na lile iliopata Chelsea katika kombe la Ligi ilipolazwa na Tottenham Hotspur.

Mchezaji wa Ghana Solomon Opaku aliekuwa akicheza kwa majaribio katika klabu ya daraja ya kwanza ya Borac Cacak huko Serbia,alijeruhiwa baada ya kuvamiwa na mashabiki waliokuwa wakimtukana kwa matusi ya kikabila mwishoni mwa mpambano wa Ligi hapo jumamosi.Taarifa hii imetolewa na vyombo vya habari vya Belgrade.

Solomon alivamiwa na washambulizi 10-gazeti la Daily Sport liliripoti leo.

Kufuatia hujuma hiyo watu 6 walitiwa nguvuni na kati yao 4 wameshtakiwa kwa makosa ya ukabila .

Kijana huyo wa Ghana alisema,

“Marafiki zangu walikuja kunichukua n a polisi akafuatana nami.Walinilinda na kupeleka hospitali.Ningependa kuruddi nyumbani haraka kama iwezekanavyo.” Alisema Opaku.

Miaka 2 iliopita ,mashabiki darzeni kadhaa wa klabu hii ya Borac walimtukana mshambulizi wa Zimbabwe Mike Tamwanjira ambae aliuhama mji huo wa Serbia baada ya kitendo hicho.Na mwaka jana tu, chama cha mpira cha Serbia kiliadhibiwa baada ya mashabiki wa Serbia walipowatukana matusi ya kikabila wachezaji weusi wa timu ya taifa ya uingereza wakati wa mashindano ya chipukizi chini ya umri wa miaka 21 ya timu za Ulaya huko Holland.Dimba la Serbia limegubikwa na mikasa na visa vya ubaguzi na kuiongoza serikali kupitisha sheria kali kupambana na mashjabiki wahuni ya kifungo cha hadi miaka 10 korokoroni.

Bingwa wa dunia wa mbio za marathon kutoka Kenya Luke Kibet aliarifu kwamba yungali anatishika baada ya kukamilisha mbio zake za kwanza tangu pale aliponusurika chupuchupu kuwawa wakati wa hujuma za mageni mwezi uliopita.Alinukuliwa kusema,

“bado siwezi kufanya mazowezi kwa utulivu kamili na hasa mapema asubuhi au magharibi.”Kibet alisema hayo baada ya kumaliza 6 katika mbio za nyika za gereza la Kenya mwishoni mwa wiki.

Zaidi ya watu 1000 miongoni mwao mwendambio za mita 400X4 katika finali ya olimpik ya 1988 mjini seoul Lucas Sang na mwendambio za marathon Wesley Ngetich wameuwawa katika machafuko ya kikabila kufuatia uchaguzi wa desemba 27 mwaka jana.

Msichana wa Ethiopia Messerat defar,bingwa wa Olimpik wa mita 5000 alishinda jana huko Stuttgart,kusini mwa Ujerumani mbio za mita 3000 kwa muda wa dakika 8:27.95 mbali sana na rekodi yake ya dunia alioiweka mjini humo mwaka mmoja uliopita.Baadae akasema, “nimevunjika moyo kidogo kwavile nimekuja hapa kwa azma ya kuivunja rekodi hiyo.” Degfar ndie mwanariadha wa mwaka uliopita wa shirika la riadha la IAAF.

Mwanariadha wa Marekani na aliekua malkia wa mbio fupi kabla kufedheheshwa kwa madhambi ya doping-Marion Jones aliripoti kwa polisi ya Texas kuanza kifungo chake cha miezi 6 kwa kusema uwongo kwa washtaki wa serikali juu ya matumizi ya madawa ya kutunisha misuli na kuongeza kasi.

Marion Jones akiwa sasa na umri wa miaka 32 amevuliwa mataji yake yote ya olimpik-matatu yakiwa ya dhahabu na ushindi wake wote mnamo mwaka 2000 umefutwa katiba madafutari.

Tukimaliza na ringi ya mabondia,Mnigeria Samuel Peter ndie mbabe wa wezani wa juu wa shirika la WBC baada ya kumdengua hapo jumamosi bingwa wa taji hilo Oleg Maskaev kwa makonde makali.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com