Stella Nyanzi atupwa mwaka mmoja unusu jela kwa kumtukana Museveni | Matukio ya Afrika | DW | 02.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

STELLA NYANZI

Stella Nyanzi atupwa mwaka mmoja unusu jela kwa kumtukana Museveni

Mahakama ya Uganda imemuhukumu mwanaharataki wa haki za wanawake, Stella Nyanzi, kifungo cha miezi 18 jela kwa kosa la kumvunjia heshima Rais Yoweri Museveni pamoja na mama wa rais huyo mkongwe zaidi Afrika Mashariki.

Kulingana na mashItaka yaliyomkabili, mhadhiri huyo wa chuo kikuu angelifungwa miaka mitatu gerezani au kutozwa faini ya shilingi millioni 1.5 za Uganda au adhabu zote mbili, lakini Hakimu Gladys Kamasanyu amemhukumu miezi 18 bila faini.

Palitokea rabsha kidogo baada ya hakimu kusoma hukumu hiyo katika ukumbi huo wa mahakama uliofurika wafuasi wa Stella Nyanzi.

Mashahidi walisema hakimu huyo alirushiwa chupa ya plastiki huku akishtumiwa kwa matamshi ya matusi, lakini walinda usalama wakadhibiti hali kwa kuwakamata baadhi ya watu.

Kwa kuwa Bibi Nyanzi alishakuwa rumande kwa miezi tisa, hukumu hii ilimaanisha kuwa sasa angelitumikia kifungo cha miezi tisa iliyobakia gerezani. Hata hivyo, wakili wake, Isaac Ssemakade, alisema angelikata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Mwaka uliopita, mwanaharakati huyo alikamatwa na kushtakiwa kwa kutumia mitandao ya mawasiliano vibaya ambapo alisambaza ujumbe uliolenga kumvunjia heshima Rais Museveni pamoja na marehemu mama yake rais huyo.

Hapakuwa na ushahidi wa kuridhisha kwamba yeye ndiye aliyesambaza ujumbe huo, lakini hakuepuka kosa la pili la kuandika ujumbe wenyewe.

Kesi dhidi ya Stella imekuwa ya vuta-nikuvute wakati hata alipomtaka Rais Museveni aje mahamani kama shahidi wake hili halikutokea.

Lubega Emmanuel/DW Kampala