1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ziarani Moscow

10 Juni 2009

Waziri wa nje wa Ujerumani akutana na rais Medvedev wa Urusi.

https://p.dw.com/p/I71v
Steinmeier na Medvedev-MoscowPicha: RIA Novosti

Waziri wa nje wa Ujerumani Bw.Frank-Walter Steinmeier, akiwa ziarani mjini Moscow, aliuambia leo uongozi wa Urusi utumie fursa iliochomoza wakati huu kupeleka mbele juhudi za kupunguza silaha za kinuklia kama ilivyopendekezwa na utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani.

Akiwa katika siku yake ya pili na ya mwisho ya ziara yake,waziri wa nje wa Ujerumani alipendekeza mwanzo mpya uchukuliwe katika maswali ya usalama na akaihimiza Urusi kufikia mapatano na Marekani kupunguza boma lao la silaha za kinuklia.

Matamshi ya waziri huyo wa nje wa Ujerumani, aliyatoa baada ya kuzungumza na rais wa Urusi Dimitry Medvedev na yamekuja wakati Moscow inajiandaa kwa ziara ya rais Obama mwezi ujao huku hatua zikiwapo kati ya dola hizo mbili kuu kufikia makubaliano ya kurefusha mkataba wao wa kupunguza makombora START kwa ufupi.

"Natumai mazungumzo hayo haraka yataleta matokeo."-alisema Bw.Frank -Walter Steinmeier.

Mkutano wa kilele baina ya rais Obama na Medvedev utakua ufunguo iwapo mwaka huu wa 2009 waweza kugeuka mwaka wa enzi mpya katika juhudi za kupunguza silaha.Bw.Steinmeier alisisitioza haja ya kuharakisha kupunguzwa kwa silaha zanuklia akitaja kesi ya Iran na Korea ya Kaskazini inabainisha wazi kwamba ulimwengu hauna muda wa kupoteza.

Baadae akihutubia Taasisi ya sayansi ya Urusi,waziri wa nje wa Ujerumani aliusihi uongozi wa Russia kuupokea mkono wa ushirikiano ulionyoshewa na Rais Obama. Alisema kusitasita kuupokea au kufanya mbinu hizi na zile kunaweza kukakomea tena mlango haraka.

katika hotuba yake Bw.steinmeier pia alizungumzia mzozo kati ya Urusi na Georgia na akaitaka Moscow kuchukua msimamo wa kujenga na sio kubomoa katika mjadala wa kuwapo vikosi vya kimataifa huko Georgia. Bw.Steinmmeier katika hotuba yake aligusia ule mzozo wa gesi kati ya urusi na Ukraine.

Bw.Frank-Walter Steinmeier,mtetezi wa wadhifa wa ukanzela kwa chama cha SPD katika uchaguzi ujao nchini Ujerumani, aliwasuili Moscow jana jioni akiwa na mazungumzo na waziri mkuu Putin na waziri wa nje Lavrov.Alisema,

"Misukosuko mingi ya kilimwengu-kuanzia mgogoro wa mashariki ya Kati hadi Afghanistan, ufumbuzi wa mzozo wa nuklia wa Iran bila ya Urusi au dhidi ya Urusi,haiwezi kusuluhishwa."

Mtayarishaji:Ramadhan Ali /DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman