1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier: Hali ni ngumu lakini Ujerumani itashinda

Mohammed Khelef
24 Desemba 2020

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani ametumia hotuba yake ya kheri za Krismasi kwa taifa kuelezea jinsi virusi vya corona vilivyoyasambaratisha maisha lakini akiwa na matumaini ya ushindi.

https://p.dw.com/p/3nB4x
Berlin I Weihnachtsansprache I Frank-Walter Steinmeier
Picha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Takribani hotuba yote nzima imejikita kwenye suala tete nchini Ujerumani na kote ulimwenguni kwa sasa - janga la virusi vya corona, ambapo ameonya kwamba bado janga la maambukizo ya virusi hivyo linaendelea kuwa kitisho kikubwa kwa maisha ya Wajerumani, ingawa amesema kuwa anatiwa moyo kuona jinsi nafsi za watu zilivyojaa umadhubuti mbele ya janga hilo.

Hotuba yake hiyo iliyoanza na swali ambalo Rais Steinmeier anasema amekuwa akitumiwa na watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakimuuliza ni lini wataweza tena kuziishi ndoto zao, inatajwa kuwa ya aina yake kutoka kwa rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani kutokana na maudhui yake kuwa ya wazi zaidi na kutawala tangu mwanzo hadi mwisho.

Kwa kawaida, mkuu huyo wa dola hutumia hotuba kama hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya kijamii, lakini mara hii hotuba nzima imekuwa ni juu ya janga la corona.

Rais Steinmeier amesema kirusi hicho kiduchu kimechukuwa umiliki wa maisha na fikira za watu, huku kikichafuwa mipango na kuharibu ndoto zao. "Mpira kwenye viwanja vya soka, sinema na matamasha ya muziki, safari za likizo, na hata sherehe za harusi, ni miongoni mwa mambo ambayo yaliyokuwa yafanyike ndani ya kipindi hiki, lakini yameshindikana," amesema Rais Steinmeier.

Kiongozi huyo amegusia pia jinsi wanafunzi wanavyokereka na familia zilizofadhaika kutokana na kulazimika kukidhi masharti ya corona kwa kusomea nyumbani na huku wakati huo huo wazazi wakilazimika kuzitunza familia zao.

"Fadhaa pia iko kwa wasanii, wasafishaji, wafanyakazi wa hoteli na wafanyabiashara za rejereja, ambao wanahofia kushindwa kabisa kuyamudu maisha kutokana na kazi zao ambazo zimeathirika sana na janga hili," amesema.

Krismasi tafauti

BdTD Deutschland "Lichtblick"-Projektion am Schloss Bellevue
Mti wa Krismasi mbele ya kasri ya rais wa Ujerumani mjini Berlin katika kipindi hiki cha corona.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kwa ujumla, Rais Steinmeier amewaambia Wajerumani kwamba Krismasi ya mwaka huu ni tafauti sana na zilizotangulia.

"Licha ya kwamba ni sherehe za kuoneshana mapenzi kwa kuwa karibu na familia na marafikki, bahati mbaya mwaka huu tunapaswa kuwa mbalimbali. Sote, nikiwemo mimi, tunawakumbuka sana marafiki na jamaa ambao hatukuweza kuwaona mwaka mzima. Wazee na wagonjwa wengi wameachwa wajiangalie na kujikinga wenyewe dhidi ya virusi," amesema kwa hisia kali.

Kwenye hotuba yake, Steinmeier amekumbusha hasa watu, wake kwa waume wanaopambana na virusi vya corona wakiwa kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi hivi sasa, majirani wanaowahofia, na wale ambao kwa bahati mbaya wameshindwa mapambano hayo na kupoteza maisha.

"Wengi wao wanakufa vifo vya uchungu mkubwa huku wakiwa wapweke na sasa hawako nasi," amesema rais huyo.

Ujerumani itashinda

Hata hivyo, Rais Steinmeier amesema kwamba jambo la kutia moyo ni kuwa janga hili limeonesha kwa jinsi gani jamii inavyoweza kuwa imara pale "tunapojaliana na kusaidiana."

Akitumia sentensi inayoshabihiana na ile kauli maarufu ya Kansela Angela Merkel ya mwaka 2015 kwamba "Tunayamudu", rais huyo amesema kwamba "nchi yetu Ujerumani ni nchi madhubuti." 

Ingawa si wazi kwamba kwa kauli hii, Steimeier alikuwa anakusudia kabisa kuchota maneno ya Merkel, ambaye aliitowa wakati akiwaruhusu maelfu ya wakimbizi na wahamiaji kuingia nchini, lakini lililo wazi ni kuwa ujumbe wao ni mmoja: nao ni kwamba Ujerumani itaishinda changamoto hii.