1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier aonya dhidi ya matamshi ya Urusi kuliimarisha jeshi lake

Josephat Nyiro Charo1 Aprili 2009

Steinmeier aitaka Urusi ichukue jukumu la kusuluhisha mizozo ya kikanda

https://p.dw.com/p/HOLJ
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema tangazo la Urusi kwamba italiimarisha kisilaha jeshi lake wakati wa upanuzi wa jumuiya ya kujihami ya NATO, limetolewa wakati usiofaa. Steinmeier pia amesema matamshi hayo ya Urusi yanatakiwa kuchunguzwa kwa makini.

Waziri Steinmeier amesema ana wasiwasi ikiwa tangazo la Urusi limetolewa wakati muafaka, akiongeza kuwa nchi hiyo ilikuwa ikipanga kwa muda mrefu kulifanyia mageuzi jeshi lake. Kiongozi huyo wa Ujerumani ameliambia shirika la habari la Reuters kwenye mahojiano yaliyofanywa kwa njia ya mtandao, kwamba likiachwa kando tangazo hilo la Urusi, kuna dalili nzuri za kutia moyo kutoka mjini Moscow na Washington kutafuta ufanisi kwenye mazungumzo ya kuachana na silaha za nyuklia.

Mbali na kuunga mkono hali ilivyo hivi sasa, waziri Steinmeier amesisitiza umuhimu wa kuyachunguza kwa makini matamshi ya serikali ya Urusi kwa mtazamo wa jumuiya ya NATO.

Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, alitangaza mwezi uliopita kwamba Urusi itaviimrisha vikosi vyake vya silaha za nyuklia na kuliimarisha na silaha mpya jeshi lake kwa sababu jumuiya ya NATO inayoongozwa na Marekani, inajipanua kuelekea mipaka ya Urusi.

Waziri Steinmeier amekuwa mtetezi mkubwa wa kufanya mdahalo na Urusi na matamshi yake yanaashiria kiwango fulani cha wasiwasi kuhusiana na mwelekeo wa matamshi ya serikali ya Moscow. Akiwa naibu kansela wa Ujerumani, Steinmeier amekuwa akichukua mkondo wa kutaka zaidi maridhiano na Urusi akilinganishwa na kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel.

Viongozi wa jumuiya ya NATO watakaokutana wiki hii katika mpaka kati ya Ujerumani na Ufaransa, wamelumbana na Urusi kuhusu maswala kadhaa katika miezi iliyopita, ikiwa ni pamoja na harakati ya jeshi la Urusi nchini Georgia mwaka jana, mzozo wake wa gesi na Ukraine, mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora na matumaini ya jamhuri za muungano wa zamani wa Sovieti, Georgia na Ukraine, kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO.

Waziri Frank Walter Steinmeier ameihimiza serikali ya mjini Moscow isaidie kutanzua mizozo ya kikanda. Aidha Steinmeier amesema Urusi inatarajiwa kuwa na jukumu muhimu katika kulainisha na kuimaliza kabisa mizozo katika eneo hilo.

Hata hivyo kiongozi huyo wa Ujerumani amekiri kwamba viongozi wa Ulaya hawawezi kusulisha maswala ya usalama barani Ulaya pasipo kuihusisha Urusi. Ndio maana lengo linabakia kujenga ushirikiano wa dhati katika kipindi kirefu, kujenga uaminifu na kutafuta njia za kushirikiana. Amesisitiza kwamba licha ya matatizo anayoyaona, hakuna chaguo lengine, na kwamba matamshi kama yale yaliyokuwa yakitolewa wakati wa vita baridi hayasaidii.

Waziri Steinmeier amezitaka nchi jirani na Urusi kuihusisha zaidi katika maswala yanayozusha ugomvi. Akizungumzia mkataba wa mwezi uliopita kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya kuhusu kuboresha mtandao wa mabomba ya gesi wa Ukraine, ambao ulizusha ukosoaji kutoka kwa Urusi kwa kuwa haikuhusishwa, Steinmeier amesema nchi zinazosafirisha nishati zinatakiwa pia kushirikishwa kwenye mazungumzo.

Wakati huo huo, waziri Steinmeier ameitetea Ujerumani kwa kushiriki katika juhudi za jumuiya ya NATO nchini Afghanistan, ambazo haziungwi mkono na idadi kubwa ya wapigaji kura hapa Ujerumani. Ameeleza umuhimu wa kuwa na uangalifu kuhusu mapendekezo ya kuwashirikisha baadhi ya wanachama wa kundi la Taliban katika juhudi za kudumisha amani nchini Afghanistan, kama ilivyopendekezwa na maafisa wa Marekani.

Kuhusu Iran, Steinmeier amesema rais wa Marekani Barack Obama ametoa ujumbe wazi alipopendekeza mwanzo mpya wa mahusiano na utawala wa mjini Tehran. Steinmeier amesema sasa ni jukumu la utawala huo kuitumia nafasi hiyo na kuongeza kuwa anatumai vikwazo zaidi havitatumika dhidi ya Iran. Amesema viongozi wa Ulaya wanatafakari hatua za kuchukua iwapo Iran itakataa pendekezo la rais Obama, lakini ni mapema mno kutoa maelezo ya kina.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: M.Abdul-Rahman