Steinmeier ahimiza mshikamano kwa wajerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Steinmeier ahimiza mshikamano kwa wajerumani

Rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema raia wa taifa hilo wanapaswa kushikamana na kukabiliana na kile kinachoweza kutajwa kuwa mzozo wa kupungua kwa imani ya umma kwa serikali.

Fernsehansprache Bundespräsident Steinmeier

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.

Kupitia hotuba ya nadra aliyoitoa kuelekea sikuuu ya Pasaka, Steinmeier amewataka wajerumani   kurejesha imani kwa serikali wakati taifa linapambana vikali na wimbi la tatu la janga la virusi vya corona.

Frank-Walter Steinmeier ambaye kwa nafasi yake kama rais asiye na nguvu wa serikali kuu ya shirikisho hushiriki shughuli nyingi za ndani na nje ya nchi, mara nyingi lakini hutoa hotuba kama hizo msimu wa sikuu ya Krismasi na siyo wakati mwingine.

Hotuba hiyo imetolewa wakati wajerumani wengi hawaridhishwi na utendaji wa serikali ikiwemo jinsi inavyoshughulikia janga la COVID-19.

Kampeni inayojikongoja ya kutoa chanjo, kukosekana kwa mshikamano wa kisiasa kulikooneshwa na uamuzi wa kansela Angela Merkel wa kubadili uamuzi wa kufungwa shughuli za kawaida wakati wa pasaka na vizuizi visivyoeleweka vya COVID-19 vyote vinawakasirisha wajerumani.

Steinmeier awarai wajerumani kuwa kuwa na imani na demokrasia

Spanien Madrid | AstraZeneca Impfstoff

Utoaji chanjo Ujerumani unakwenda kwa mwendo wa konokono

Steinmeier amesema watu “wameendelea kuchanganyikiwa na kuhisi hawana msaada” hali iliyosababisha kuzuka hali ya shaka shaka nchini Ujerumani.

Kiongozi amewataka watu kuwa na imani na mfumo wa demokrasia ambao ni mkataba baina ya umma na serikali ambao unawezesha kila upande kutimiza wajibu.

Rais Steinmeier amesema kupungua imani ya umma kwa serikali yao ni mzigo mwingine ukiachilia wasiwasi kuhusu afya, elimu, kazi na uchumi ambavyo vimekuwa vikitawala ajenda za siasa katika kushughulikia kadhia ya corona.

Kupitia hotuba Steinmeier amekiri kuwa Ujerumani ilifanya makosa "katika kupima, kutoa chanjo na matumizi ya teknolojia”, kupambana na janga la COVID-19 na kwamba raia wanayo haki ya kuwaambia viongozi wao kuwa wana wajibu wa kufanya vizuri zaidi.

"Bila shaka hakuna njia moja ya kumaliza ugonjwa wa mlipuko. Na ndiyo maana tunahitaji mjadala wa kisiasa-lakini mjadala huo haupaswi kuwa ndiyo hitimisho lenyewe.” amesema Steinmeier.

Steinmeier: Nina imani na kila chanjo

Coronavirus - Impfung Bundespräsident Frank-Walter Steinmeier

Steinmeier akipatiwa chanjo ya COVID-19.

Steinmeier amezungumzia pia imani aliyo nayo kwa kila chanjo iliyoidhinishwa nchini Ujerumani.  Kiongozi huyo ameongeza kusema utoaji wa chanjo ni hatua muhimu kwenye njia ya kumaliza janga la corona na kuwatolea wito wajerumani kujitokeza ili kuchanjwa.

Rais Steinmeier alipatiwa dozi ya kwanza ya chanjo ya AstraZeneca Alhamisi iliyopita. Chanjo hiyo imekuwa kitovu cha wasiwasi kufuatia madai kuwa inasababisha kuganda kwa damu licha ya shirika la afya duniani WHO na wakala wa dawa wa Ulaya kuwaondoa watu wasiwasi.

Fadhaa na Hamkani zinaeleweka

Steinmeier ametumia hotuba yake kuonesha huruma kwa watu wanaoishi Ujerumani katika kipindi hiki cha janga. ``Ninafahamu, mnafanya kila mnaloweza katika mzozo huu wa kihistoria. Mnaweka kila juhudi na kuweka rehani mambo mengi. Baadhi yenu, suala siyo tena kuhusu fedha mlizopoteza wakati wa kufungwa kwa shughuli za kawaida, bali kuhusu iwapo mtaweza tena kusimama kifedha`` amesema Steinmeier.Akihitimisha hotuba yake Steinmeier amezungumzia fahari ya Ujerumani kwa jinsi taifa hilo lilivyoongoza juhudi chungunzima za kukabiliana na janga la virusi vya corona tena kwa mafanikio katika kipindi cha miezi ya mwanzo ya janga hilo. Amesema hata kama Ujerumani haitokuwa kinara wa kupambana na COVID-19 pia haitakuwa muhanga mkubwa wa kadhia hiyo.