Steinbrück aongeza kasi dakika za mwisho | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 11.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Steinbrück aongeza kasi dakika za mwisho

Mgombea ukansela wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani , Social Demokratik, bwana Peer Steinbrück ameyajibu maswali kadhaa juu ya uchaguzi katika mji wa magharibi wa Mönchengladbach.

Mgombea Ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrück

Mgombea Ukansela wa chama cha SPD ,Peer Steinbrück

Mgombea Ukansela wa chama cha SPD Bwana Steinbrück amejibu maswali hayo kwenye mhadhara uliotangazwa moja kwa moja kwenye televisheni kutokea mji huo wa magharibi wa Mönchenglabach. Alizungukwa na jopo la wapiga kura 150 wakati wa kuyajibu maswali kwa muda wa saa moja na robo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaewania muhula wa tatu alizungumza kwenye televisheni jumatatu iliyopita. Kwa mujibu wa kura za maoni Kansela huyo ambae ni mwenyekiti wa chama cha CDU kinachoiongoza serikali ya Ujerumani bado anayo matumaini ya kushinda vizuri. Hata hivyo mpinzani wake Bwana Steinbrück amepanda juu kidogo katika kura za maoni wakati siku ya uchaguzi inakaribia, hapo tarahe 22. Vyama ndugu vinavyoongoza serikali CDU na CSU vinatarajiwa kupata asilimia 39 ya kura wakati chama cha Bwana Steinbrück ,SPD kinatarajiwa kufikia asilimia 25.

Vyama vya upinzani havina turufu

Vyama vya upinzani mpaka sasa havijafanikiwa kuzungumzia suala linaloweza kuigeuza misimamo ya wapiga kura ingawa katika mjadala wa kwanza kwenye televisheni, septemba mosi ,mgombea wa chama cha SPD Peer Steinbrück aliweka mkazo juu ya masuala ya kijamii katika hoja zake.Bwana Steinbrück amesema ,ikiwa atachaguliwa atachukua hatua za haraka kuleta mabadiliko nchini Ujerumani. Amesema dhamira yake endapo atakuwa Kansela wa Ujerumani, ni kuanzisha mabadiliko ya kisiasa mara moja nchini Ujerumani.

Miongoni mwa hatua za kwanza ambazo Steinbrück ameahidi kuzichukua endapo atachaguliwa kuwa Kansela wa Ujerumani ni kupunguza kodi ya nishati ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za maisha.

Tokea kupambana kwa hoja na Kansela Merkel kwenye televisheni septemba mosi bwana Steinbrück ameweza kujiongezea alama .Lakini cha SPD bado kipo nyuma, licha ya bwana Steinbrück kuweza kujiongezea alama sita.

Merkel bado imara

Akihutubia jumatatu iliyopita Kansela Merkel pia aliyazungumzia masuala ya kijamii.Alionyesha mshikamano juu ya watu wenye kazi za mishahara ya chini.Bibi Merkel pia amewaahidi wananchi kwamba Ujerumani haitashiriki katika mpango wa Marekani wa kuishambulia Syria.

Wakati zimebakia siku chache kufikia uchaguzi mshirika mkuu wa SPD, chama cha kijani kimerudi nyuma katika umaarufu. Taasisi ya utafiti ya Forsa imeonyesha kuwa chama cha kijani kimerudi nyuma kwa alama mbili hadi kufikia asilimia 9 ,nyuma ya chama cha mrengo wa shoto chenye asilimia 10.Na endapo uchaguzi ungelifanyika leo,mshirika wa Kansela Merkel chama cha Waliberali, FDP kingelipata asilimia sita ya kura.

Mwandishi:Mtullya Abdu /dpa,afp.

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com