Standard & Poors yaushusha uwezo wa Uhispania kukopesheka | Masuala ya Jamii | DW | 11.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Standard & Poors yaushusha uwezo wa Uhispania kukopesheka

Wakala wa viwango wa Standard & Poors umeushusha uwezo wa Uhispania kukopesheka hadi kiwango cha chini kabisa, hali inayotishia kuwa nchi hiyo nayo inaweza kutumbukia kwenye mzozo wa madeni hivi punde.

Sarafu ya euro.

Sarafu ya euro.

Standard & Poors inasema dhamana za serikali ya Hispania zimeshuka kutoka BBB+ hadi BBB- na sasa deni la nchi hiyo limebakia hatua moja kufikia kiwango cha kutolipika tena. Uwezekano wa uwezo huo kushushwa zaidi ni mkubwa.

Wakala huo wenye makao yake makuu New York, Marekani, umesema hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa hali mbaya kiuchumi na kisiasa, katika taifa hilo la nne kwa uchumi mkubwa katika kanda ya euro. Hali hii inamaanisha kupunguza nguvu za serikali kupatana na taasisi za kifedha.

Katika taarifa yake, Standard & Poors imesema kupanda kwa idadi ya wasio na ajira na makato ya mshahara kwa walio nayo kutaongeza machafuko ya kijamii na kuimarisha mivutano kati ya serikali kuu mjini Madrid na zile za majimbo.

Wakala huo wa viwango umesema kwamba maendeleo katika kanda ya euro yanachangia katika kuporomoka uwezo wa Uhispania kukopesheka. Mashaka juu ya uwezo wa Uhispania kurekebisha madeni ya benki zake yataathiri sana mtazamo wa mikopo kwa nchi hiyo.

Hali kuzidi kuwa ngumu

Waziri wa uchumi wa Uhispania, Luis de Guindos (kushoto), akizungumza na mwenzake wa Luxembourg, Jean-Claude Juncker.

Waziri wa uchumi wa Uhispania, Luis de Guindos (kushoto), akizungumza na mwenzake wa Luxembourg, Jean-Claude Juncker.

Kukosekana kwa muongozo wa kisera katika kanda ya euro kunahujumu muonekano wa kiwango cha madeni, wamesema Standard & Poors.

Uhispania imekuwa ikipokea msaada kwa benki zake kutoka kanda ya euro, ingawa hadi sasa serikali ya Waziri Mkuu Mariano Rojoy haijaomba rasmi msaada kutoka mfuko wa uokozi wa Umoja wa Ulaya.

Uchumi wa Uhispania unayumba sana na benki zake zinapigana kujiinua baada ya kuporomoka kwa soko la nyumba nchini humo, ambalo lilikuwa uti wa mgongo wa sekta ya benki.

Benki Kuu ya Ulaya imekubali kununua dhamana za madeni ya Uhispania ili kusaidia kushusha gharama za ukopaji, lakini kwanza serikali inapaswa kuomba msaada wa uokozi.

Masoko ya hisa Ulaya yatikisika

Maandamano dhidi ya kubana matumizi Uhispania.

Maandamano dhidi ya kubana matumizi Uhispania.

Tayari athari za tangazo la kushushwa uwezo wa Uhispania kukopesheka, zimeanza kuonekana kwenye masoko. Hisa za Ulaya zimeshuka kwa kipindi cha nne mfululizo hivi leo. Faharasa ya FTS Eurofirst inaonesha kuporomoka kwa asilimia 0.1, huku ile ya Euro STOXXX ikishuka kwa asilimia 0.5.

Katika hatua nyengine kwenye mgogoro wa madeni katika kanda ya euro, Ugiriki itahitaji miaka mingine miwili kabla ya kusimama sawasawa kiuchumi. Hayo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, Christine Lagarde.

Lagarde amewaambia waandishi wa habari mjini Tokyo kwamba itachukua muda zaidi kwa serikali ya Ugiriki kupunguza nakisi ya bajeti kufikia viwango vilivyokubaliwa.

Hivi sasa Ugiriki inapitia kipindi kigumu kabisa cha kubana matumizi na mageuzi ya kiuchumi inayolazimika kuyafuata ili kupata mkopo na nafuu ya deni yenye thamani ya euro bilioni 347.

Hatua hizo za kukaza mkanda zimeilazimisha nchi hiyo kuingia mwaka wa tano wa kuporomoka kiuchumi. Mtu mmoja katika kila watano nchini Ugiriki hana kazi na wengi wa wale wenye kazi wanakatwa mishahara yao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com