Staffan de Mistura kujiuzulu mwezi Novemba | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.10.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Staffan de Mistura kujiuzulu mwezi Novemba

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria, Staffan De Mistura, ametangaza siku ya Jumatano kwamba atajiuzulu mwishoni mwa mwezi ujao wa Novemba kutokana na sababu za kibinafsi.

De Mistura amesema anajiuzuku ili awe na muda na familia yake. "Sababu za kibinafsi za kujiuzulu si afya, ni familia kimsingi," alisema de Mistura wakati alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York. "Kwa hiyo hakuna haja ya kubahatisha kuhusu hilo. Mimi ni mzima sina neno na hata sijachoka, kwa sababu kazi hii imekuwa ikinitia tumbo joto, kibarua cha aina hii," akaongeza kusema mjumbe huyo mwenye umri wa miaka 71. 

Raia huyo wa Italia mwenye asili ya Uswisi alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mchakato wa kisiasa unaendelea, licha ya kwamba serikali ya Syria imeyakomboa maeneo mengi ya nchi.

De Mistura, ambaye amekuwa katika wadhifa huo kwa zaidi ya miaka minne, ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba katibu mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres, alikuwa amemuagiza kuhakiki kwa ukamilifu iwapo kamati ya kuaminika ya masuala ya katiba inayowajumuisha wajumbe wa pande zote inaweza kuundwa.

De Mistura ndiye mpatanishi aliyehudumu muda mrefu Syria

De Mistura ndiye mpatanishi aliyehudmu kwa muda mrefu zaidi kati ya wapatanishi watatu wa Umoja wa Mataifa waliohudumu wakati wa zaidi ya miaka saba ya mzozo wa Syria. Watangulizi wake, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, marehemu Kofi Annan na mwanadiplomasia mkongwe kutoka Algeria Lakhdar Brahimi, wote walijiuzulu baada ya kukatishwa tamaa kutokana na mkwamo wa kimataifa kuhusu jinsi ya kuvifikisha mwisho vita nchini Syria.

Syrien - Präsident al-Assad trifft Kofi Annan in Damaskus

Kofi Annan alipokutana na rais wa Syria Bashar al Assad mjini Damascus 09.07.2012

Wanadiplomasia walisema miongoni mwa watu wanaofikriwa huenda wakajaza pengo litakaloachwa na de Mistura ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jan Kubis, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Algeria, Ramtane Lamamra, mjumbe wa Umoja wa Mataia kwa ajili ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov na balozi wa Norway nchini China, Geir Pedersen.

Washiriki katika mkutano kuhusu amani ya Syia uliofanyika nchini Urusi mwezi Januari mwaka huu walikubaliana kuunda kamati ya katiba itakayowajumuisha watu 150, huku theluthi moja kati yao wakichaguliwa na serikali, theluthi moja nyingine ikichaguliwa na makundi ya upinzani na theluthi ya mwisho na Umoja wa Mataifa.

Mchakato wa kuunda jopo la katiba umechelewa

De Mistura alisema kuundwa kwa jopo hilo kulikuwa kumecheleweshwa huku maswali yakiendelea kuulizwa, hususan na serikali ya Syria, kuhusiana na majina ya watu watakaojumuishwa katika orodha ya Umoja wa Mataifa. Alisema atafanya ziara mjini Damascus wiki ijayo na ana matumaini ya kuishawishi serikali kuridhia na kuidhinisha orodha ya tatu itakayowajumuisha wajumbe kutoka pande zote.

"Kukiwa na ari ya kisiasa, hakuna sababu ya kuzuia kamati ya katiba kuundwa mwezi Novemba," alisema de Mistura wakati alipolihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lenye nchi 15 wanachama, na ambalo kwa muda mrefu limekabiliwa na mkwamo kutoka na vita vya Syria, huku nchi za magharibi zikiwa na msimamo unaokinzana na Urusi, ambayo ni mshirika wa Syria.

UN - Francois Delattre

Francois Delattre, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Francois Delattre, ameishutumu serikali ya Syria kwa kuzuia kuundwa kamati hiyo, hatua ambayo hatimaye inawadhihirishia kuwa haitaki kushiriki katika jitihada za kidiplomasia zinazoendelea, wakati washirika wake wakiwa hawawezi au hawataki kuishawishi ifikishe kikomo vita hivyo.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, alisema Urusi inataka kamati ya katiba iundwe haraka iwezekanavyo lakini kuweka tarehe ya mwisho ambapo kamati hiyo inatakiwa iwe imeunda, itakuwa sawa na kutwanga maji kwenye kinu. "Ili mchakato uweze kuaminika, basi lazima pawepo makubaliano kati ya pande zote na itachukua muda. Kwa hiyo tunahitaji kuwa wavumilivu," alisema Nebenzia.

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, alisema serikali ya Syria imejitolea kwa dhati katika mchakato mzima wa kuundwa jopo la katiba.

Mwandishi: Josephat Charo/reuters