Spain imerudi nyumbani na Kombe la dunia kama pweza Paul alivyoagua. | Michezo | DW | 12.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Spain imerudi nyumbani na Kombe la dunia kama pweza Paul alivyoagua.

Holland mara 3 makamo-bingwa yafuta tena machozi.

Spain washangiria ushindi wa kombe la dunia.

Spain washangiria ushindi wa kombe la dunia.

Mabingwa wa ulaya-Spain , ndio mabingwa wapya wa dunia :Katika finali kati ya Pweza wa Ujerumani, Paul na pweza wa Holland, Pauline, pweza wa Ujerumani,ameshinda finali yao kwvile hakukosea tena kuagua. Holland kwa mara ya 3 ni makamo-bingwa.

Ujerumani,imerudi leo nyumbani ikiwa ni mshindi 3 na chipukizi wake Thomas Mueller, sio tu mtiaji mabao mengi kabisa katika Kombe hili la dunia ,bali ndie alievalishwa taji la "stadi bora chipukizi" 2010 akiwapiku Andrew Ayew wa Ghana na Dos Santos wa Mexico. Diego Forlan, wa Uruguay,ndie "mchezaji-bora " wa Kombe la dunia 2010.Mzee Mandela,alifika uwanjani City Stadium, kuliaga Kombe la kwanza la dunia barani Afrika, huku mrembo Shakira,akitumbuiza mashabiki kwa "waka waka".

SPAIN 1 HOLLAND 0

Katika finali ya timu 2 pekee za ulaya-Spian na Holland,haukua mchezo wa kusisimua,bali vita uwnajani na kutiana miereka tu.Jumla ya kadi 13 za manjano za maonyo -8 kwa Holland na 5 kwa Spain ,zilitolewa na rifu wa Uingereza na mwishoe, maji yalipozidi unga, alimtimua nje John Heitinga, alipobidi kumkabidhi kadi nyekundu awage uwanja.

Mashabiki wa Spain wakaangua vilio kwa furahaa baada ya hodi-hodi zao nyingi katika lango la wadachi,mwishoe, kuitikiwa dakika chache kabla ya firimbi ya mwisho ya kipindi cha ziada.

Kufuatia ushindi wa Spain, wa kwanza wa Kombe la dunia katika historia ya miaka 80 ya kombe hili,ikawa "asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu alitia gongo",wakubwa kwa wadogo,wake kwa waume,walimiminika uwanjani Johannesberg, mitaani nchini Spain na hata Ujerumani,wakipiga mayowe na kupuliza vuvuzuela. Umati wa mashabiki 90.000 uwanjuani,uliwashangiria waspain kwa vuvuzela na mayowe.Magombe dume, ni waflame wa dinmba wa dunia na Gombe-dume lao ni Andres Iniesta.

Huko Holland, kila kitu kilipooza kana kwamba, nchi nzima imefiwa.Na hii yafahamika, kwani, ni mara ya tatu baada ya 1974 Ujerumani na 1978 huko Argentina, Holland, inabidi kuridhika na taji la makamo-bingwa.

Huzuni za wadachi,hazikuweza kugubika furaha ya kiasi cha waafrika bilioni 1 kwa jinsi walivyoliandaa Kombe lao la kwanza la dunia.Wengi wanajivunia licha ya kwamba timu zao 6 hazikutamba kama ilivyotazamiwa.

Sasa Afrika inadai kuandaa Olimpik barani Afrika na Rais wa FIFA Sepp Blatter,ameahidi kuliungamkono bara la Afrika katika hilo.

Wakati Spain na Holland, wamegawana nafasi ya kwanza na ya pili, Ujerumani,mojawapo ya timu zilizosisimua mno katika Konbe hili la dunia,imerudi nyumbani mapema leo asubuhi.Ndege ya LUFTHANSA ilitua uwanja wa ndege Frankfurt,huku mashabiki kadhaa wakifika kuwalahki lakini bila ya mafanikio.

"Tumevunjwa moyo kuwa hawakujali hata kutupungia mkono na wametupita tu wakienda zao." - Walilalamika mashabiki hao wa kike wa Ujerumani,iliomaliza nafasi ya 3 kwa kuilaza uruguay, jumamosi usiku mabao 3:2.

Nae makamo-nahodha wa Ujerumani ,stadi wa kiungo Bastian Schweinsteiger, alijibu manun'guniko hayo ya mashabiki:

"Kila mchezaji amevunjika moyo kwa kutokea 3.Tungependa sana kurudi na Kombe na hapo tena tungefurahia kusherehekea pamoja na mashabiki."

Baada ya kurejea kikosi cha Ujerumani kutoka Kombe la dunia, swali linaloulizwa wakati huu ni je, kocha Joachim Löw,ambae juzi alitunukiwa nishani kuu ya Ujerumani ya ufanisi na rais Christian Wulff,aliekuwapo uwanjani huko Port Elizabeth, wakati wa mpambano wa kusaka mshindi 3 na jana siku ya finali huko City Stadium, atabakia kuwa kocha wa Ujerumani ?

Kulikuwapo na mvutano na Shirikisho la dimba la Ujerumani juu ya masharti ya mkataba wake. Löw ameomba muda kuzingatia siku zake za usoni.Wengi wanatazamia kwamba, atabakia kuwa kocha wa Ujerumani na kuiongoza hadi finali za Kombe lijalola ulaya 2012 huko Poland na Ukraine, ambako Ujerumani imepanga kuivua taji Spain.

Kulikuwa na finali 2 za Kombe la dunia hapo jana: kwa upande mmoja, ilikuwa kati ya Spain na Holland na upande wapili, ilikuwa kati ya pweza Paul wa Ujerumani na Pauline -pweza wa Holland. Paul,alitabiri kwamba, Spain ingetoroka na Kombe kama alivyoagua kabla kwamba, ingeitoa Ujerumani. Wadachi hawakuridhika na utabiri wa Paul,wakamuuliza -Pauline maoni yake.Yeye akawaambia "Paulo "kakosea.

Changamoto yao majini ilikwenda hadi dakika ya 116 ya mchezo ,na mwishoe, Pauline wa Holland, akabidi kuungama Paulo hakosei.

Mabingwa wa dunia -Spain, wakiwa wameshawasili Madrid, alaasiri ya leo na Kombe lao kutoka Afrika kusini kulitembeza mjini Madrid na kwa Qasri la mfalme Juan Carlos, Rais wa FIFA-Sepp Blatter, alitoa leo pongezi kwa wenyeji Afrika Kusini kwa kuandaa uzuri Kombe la dunia 2010. Akaueleza ushindi wa Spain dhidi ya Holland kuwa ni ushindi wa dimba.Alipoulizwa kukadiria jinsi Afrika Kusini ilivyoandaa Kombe la dunia,Blatter alisema walipoandaa Kombe la Mashirikisho, Afrika Kusini walistahiki alama 7.5 katika 10 mara hii katika Kombe la dunia wamestahi alama 9/10.

Kombe la dunia 2014 ni zamu ya samba huko Copa Cabana, Brazil.Afrika nzima inatoa salamu za vuvuzela na "waka waka " na kuiambia -Rio-tunakuja kwa kishindo ."

Mwandishi:Ramadhan Ali /DPAE

Uhariri: Abdul-Rahman