Somalia:Mapigano yasita kwa muda , Uganda na Eritrea zajadili amani. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 02.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Somalia:Mapigano yasita kwa muda , Uganda na Eritrea zajadili amani.

Mamia ya wanajeshi wa ziada kutoka Ethiopia waliingia mjini Mogadishu leo Jumatatu , baada ya siku nne za mapigano makali yaliyozuka kutokana na mashambulizi ya majeshi hayo ya Ethiopia dhidi ya waasi wa Kiislamu na makundi ya kiukoo yanayopigana nchini Somalia.

Mtu mmoja akipita karibu na gari la jeshi lililoungua moto,wakati jengo moja likifuka moshi kutokana na mapigano nchini Somalia.

Mtu mmoja akipita karibu na gari la jeshi lililoungua moto,wakati jengo moja likifuka moshi kutokana na mapigano nchini Somalia.

Wakaazi katika maeneo ya vitongoji vya mji wa Mogadishu wamesema kuwa majeshi ya ziada kutoka Ethiopia yaliingia katika mji huo mkuu yakitokea upande wa njia itokayo Baidoa, ambako serikali ya mpito hadi sasa ina makao yake makuu.

Majeshi ya Ethiopia pamoja na zana zake za kivita bado zimewekwa katika kitongoji cha Ali Kamin , karibu na uwanja mkuu wa mpira, ambako mapigano yalikuwa makubwa zaidi na milio ya bunduki ya hapa na pale bado imeendelea kusikika hadi leo asubuhi.

Hakuna idadi kamili inayojulikana ya watu waliopoteza maisha kutokana na mapigano hayo tangu pale majeshi ya Ethiopia yalipoanzisha mashambulizi yao dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu kwa nia ya kuwaondoa kutoka katika mji huo mkuu siku ya Alhamis, lakini shirika la misaada la msalaba mwekundu linakadiria kuwa dazeni kadha za raia wameuwawa.

Shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema jana Jumapili kuwa kiasi cha watu 47,000 wamekimbia kutoka mji mkuu Mogadishu katika muda wa siku kumi zilizopita kutokana na mapigano hayo.

Shirika hilo limeongeza kuwa watu 96,000 wamekimbia makaazi yao mjini Mogadishu mwezi wa February na March. Shirika la habari la Reuters pia limeona milolongo mirefu ya watu wakiukimbia mji huo mkuu, baadhi wakitembea kwa miguu, na wengine wakiwa wamebeba vitu vyao kwa punda, magari madogo na malori.

Wazee kutoka katika ukoo maarufu katika mji huo mkuu wa Hawiye, jana walitoa wito wa kumalizwa mapigano, ambayo wachunguzi wa kimataifa wanasema kuwa yalikuwa mabaya zaidi katika muda wa miaka 15 nchini humo, lakini majeshi ya Ethiopia hayajasema lolote kuhusu jaribio la pili la kufikia mapatano katika muda wa wiki mbili zilizopita.

Wazee hao wameyataka majeshi ya umoja wa Afrika ya kulinda amani , ambayo yanawanajeshi wapatao 1,500 mjini Mogadishu , kuangalia utekelezaji wa usitishaji wa mapigano. Mwanajeshi mmoja wa jeshi la umoja wa Afrika kutoka Uganda aliuwawa na wengine watano wamejeruhiwa mwishoni mwa juma , ikiwa ni kifo cha kwanza miongoni mwa wanajeshi wa jeshi la kulinda amani la umoja wa Afrika walioko nchini Somalia.

Naibu waziri wa ulinzi katika serikali ya mpito nchini Somalia Salad Ali Jelle amewataka raia wanaoishi katika maeneo yanayohusika katika mapigano kuhama maeneo hayo wakati majeshi ya serikali pamoja na yale ya Ethiopia yakifanya mashambulio makali dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu. Salad Ali Jelle amesema kuwa serikali yake haitambui makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya majeshi ya Ethiopia na wazee wa koo maafuru mjini humo. Akaongeza kuwa raia wote wanaoishi katika maeneo yanayoshikiliwa na magaidi wanatakiwa kuondoka katika maeneo hayo kwa sababu inawezekana majeshi ya serikali yakashambulia maeneo hayo.

Viongozi wa mataifa ya Eritrea na Uganda wakati huo huo wamekuwa na mazungumzo leo kuhusiana na hali inayozidi kuwa mbaya nchini Somalia. Rais wa Eritrea Issaias Afeworki na rais Yoweri Museveni wa Uganda wamekuwa na mazungumzo yao mjini Massawa nchini Eritrea.

Wakati huo huo wakaazi wa mji wa Mogadishu wamekuwa wakizika maiti za watu waliokufa leo na baadhi kuingia katika mitaa ya mji huo kwa mara ya kwanza katika muda wa siku tano, baada ya mapigano kusita.

 • Tarehe 02.04.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4y
 • Tarehe 02.04.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4y

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com