Somalia yatimiza miaka 20 bila Barre | Matukio ya Afrika | DW | 26.01.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Somalia yatimiza miaka 20 bila Barre

Tarehe 26 Januari dikteta Mohamed Siad Barre wa Somalia alilazimika kuacha madaraka yake na tangu wakati huo nchi hiyo imetumbukia katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe, huku ikikosa serikali imara hadi sasa.

Mohammed Siad Barre

Mohammed Siad Barre

Mohammed Siad Barre aliitawala Somalia kwa zaidi ya miaka 20. Katika enzi za Vita Baridi alikuwa kwanza kipenzi cha kambi ya mashariki na baadaye akageuka kuwa kipenzi cha magharibi. Nchini Ujerumani Mohamed Siad Barre alijipatia umaarufu kutokana na opereshini ya kukombolewa ndege ya shirika la ndege la Lufthansa iliyokuwa imetekwa nyara na magaidi.

Alipolazimika kuwachia madaraka, vurugu likatawala nchini Somalia. Vita vya miongo vya wenyewe kwa wenyewe vikaripuka. Mpaka leo nchi hiyo haina serikali imara, badala yake wafuasi wa itikadi kali ya dini ya Kiislam wanadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na, ikiwa kuna chochote kilichopatikana, basi ni nchi hiyo ya pembe ya Afrika kugeuka ngome ya maharamia.

Barre alichoshwa na malumbano ya kisiasa

Wanajeshi wa Kimarekani wakimwadhibu kijana wa Kisomali mwaka 1992

Wanajeshi wa Kimarekani wakimwadhibu kijana wa Kisomali mwaka 1992

Mapema mwaka 1990, katika mahojiano yake ya mwisho na kituo cha televisheni cha Ujerumani, ARD, Mohammed Siad Barre akivalia kama desturi yake sare ya kijeshi na miwani ya jua alisema ameshachoshwa na mapambano ya kisiasa.

Siad Barre aliingia madarakani mwaka 1969 kufuatia mapinduzi ya kijeshi na akaanza kutawala kimabavu. Picha za televisheni kuhusu Wasomali waliokondeana na wengine wanaokufa kwa njaa ziliwahuzunisha walimwengu. Umoja wa Mataifa ukaingilia kati. Rais wa Marekani wa wakati ule George Bush alisema, jumuiya ya kimataifa ilikuwa na sababu moja tu ya kwenda Somalia.

"Tunataka kuwahudumia wanaosumbuliwa kwa njaa, kuwasaidia wayanusuru maisha yao. Marekani lazima iwajibike."

Msako wa Aidid ulivyoigeuka Marekani

Somalia haijatawalika tena

Somalia haijatawalika tena

Lakini mkasa wa Marekani kuingia Somalia nusura ugeuke kashfa nyengine ya Vietnam kwa nchi hiyo. Mohammed Farah Aidid, mbabe wa kivita aliyekuwa na nguvu kuliko wote mjini Mogadishu alipania kuwatimuwa wanajeshi wa Marekani.

Oktoba 1993, balaa kubwa likazuka. Aidid alifanikiwa kuzidungua helikopta tatu za kivita za Marekani. Wanajeshi 18 wa Marekani wakauliwa, Wasomali kadhaa wakaiburura maiti ya mwanajeshi mmoja wa Marekani majiani katika barabara zilizojaa mavumbi, tena bila ya kujali kamera za televisheni ya CNN .

Huo ukawa mwanzo na mwisho wa kuwepo vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Somalia na Marekani kuapa haitotia tena mguu wake nchini humo.

Tangu wakati vurugu inatawala. Hata serikali ya mpito inayoungwa mkono na Umoja wa Afrika haina nguvu za kutosha. Sehemu kubwa ya nchi hiyo inadhibitiwa na waafuasi wa itikadi kali ya dini ya Kiislam, Al-Shabbab.

Mwandishi: Diekhans Antje/Nairobi (WDR)/Hamidou Oummil
Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza