Somalia yadai imewafurusha wanamgambo kutoka Mogadishu. | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Somalia yadai imewafurusha wanamgambo kutoka Mogadishu.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imearifu kiasi watu laki nne yamkini wameukimbia mji mkuu Mogadishu, Somalia kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo. Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, John Holmes, amewaambia waandishi wa habari hali nchini Somalia inasikitisha kwa misingi ya kibindamu. Kwa mujibu wa John Holmes, wanawake, watoto na wazee ndio ambao wamekuwa wakikimbia vita hivyo vinavyoendelea katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Wanamgambo wa Kiislamu wajiandaa kuvishambulia vikosi vya serikali nchini Somalia.

Wanamgambo wa Kiislamu wajiandaa kuvishambulia vikosi vya serikali nchini Somalia.

Wakati idadi ya watu wanaokimbia Mogadishu ikitangazwa kuwa imeongezeka, Waziri Mkuu wa Somalia, Ali Mohamed Gedi ametangaza kwamba majeshi ya serikali yamewashinda wanamgambo wa Kiislamu mjini Mogadishu baada ya mapambano yaliyodumu kwa muda wa siku tisa.

Mamia ya watu wameuawa kwenye mapigano hayo yaliyokuwa makali ambapo wanamgambo wa kiislamu pamoja na wanajeshi wa serikali wanaoungwa mkono na Ethiopia walikabiliana kwa vifaru pamoja na magari ya kijeshi.

Ingawa waziri huyo mkuu aliwaambia waandishi wa habari kwamba harakati kuu za kijeshi zimekamilika, milio ya risasi ilikuwa ikisikika katika mji huo ulioharibiwa na vita na unaokadiriwa kuwa na wakazi milioni mbili.

Waziri Mkuu Mohamed Gedi amewatolea wito watu kiasi laki tatu na elfu arobaini walioukimbia mji wa Mogadishu kutokana na vita hivyo, kuanza kurejea makwao.

Mapigano hayo ndio makali zaidi kuwahi kutokea tangu miaka kumi na mitano iliyopita.

Mratibu wa shughuli za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, John Holmes, amesema mapigano yameongezeka kama siku kumi hivi zilizopita na kuwatatiza wakazi kwa kiasi kikubwa.

John Homes amesema shirika lake tayari linawalisha watu milioni moja.

Hata hivyo mratibu huyo anasema harakati za kijeshi zinazoendelea nchini humo zimetatiza shughuli za wafanyikazi wa kutoa misaada.

"Imekuwa vigumu kuwafikia waathiriwa kwa sababu tulikosa kuelewana na wakuu wa serikali za mitaa. Serikali ya mpito ya Somalia haijashirikiana nasi jinsi ambavyo tulitarajia kwani hatujaweza kutumia viwanja vya ndege mjini Mogadishu wala hatukutaka kutumia Uwanja Mkuu. Tumesumbuka sana wakati tukiomba kibali"

Kulingana na wakazi wa Mogadishu, wanamgambo wa kiislamu wamesitisha makabiliano ya ana kwa ana na yamkini wanajikusanya ili kuanza upya mapambano.

Wakazi hao wamesema wanajeshi wa Ethiopia wamewafurusha wanamgambo kutoka ngome zao muhimu hasa kizuizi cha barabarani cha Balad ambacho ni muhimu kwa uchukuzi wa mahitaji ya wanamgambo hao.

Serikali ya mpito ya Somalia imewataka wanamgambo hao kujisalimisha huku ikidai kufikia mwishoni mwa juma hili itakuwa imechukua mamlaka ya mji wa Mogadishu.

Wafanyikazi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu walioko nchini Somalia wamesema watu mia tatu na ishirini na tisa wengi wao wakiwa raia pamoja na wanamgambo wa kiislamu, wameuawa tangu kutokea kwa mapigano ya hivi karibuni.

Wakati huo huo, Shrika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula limeanza kugawa chakula kwa raia waliokimbia makazi yao katika maeneo sita mjini Mogadishu na viunga vyake.

Kulingana na wafanyikazi wa mashirika ya kutoa misaada, maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wamepiga kambi katika maeneo ya karibu na Mogadishu na wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa maradhi, hawana maji, chakula wala dawa za kutosha.

 • Tarehe 26.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHFO
 • Tarehe 26.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHFO

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com