Somalia na matumaini ya enzi mpya kwa Hassan Sheikh Mohamud | Matukio ya Afrika | DW | 11.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Somalia na matumaini ya enzi mpya kwa Hassan Sheikh Mohamud

Wabunge wa bunge la Somalia waliandika historia mpya Jumatatu kwa kumchagua mwanataaluma Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais mpya wa nchi hiyo, katika matokeo yaliyoelezwa kama kura ya mabadiliko katika nchi hiyo.

Hassan Sheikh Mohamud, rais mpya wa Somalia.

Hassan Sheikh Mohamud, rais mpya wa Somalia.

Nderemo na vifijo vilitawala anga la Mogadishu baada ya kutangazwa kwa matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi huu wa aina yake nchini Somalia. Mohamud alishinda kura hiyo ya siri kwa kuungwa mkono na wabunge 190 dhidi ya 79 waliompigia kura rais aliyekuwa madarakani Sheikh Sharif Ahmed, ambaye hapo awali alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo. Mohamud alishika nafasi ya pili katika wagombea 25 wa duru ya kwanza, kwa kupata kura 60 dhidi ya 64 za Sheikh Sharif Sheikh Ahmed.

Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed.

Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed.

Rais huyo mpya ambaye kama Sheikh Sharif Ahmed, anatokea katika kabila la Hawiye, anahusishwa na chama cha Al-Islah ambacho ni tawi la Somalia la Chama cha Udugu wa Kiislamu. Baada ya kutangazwa mshindi, Mohamud alisema kilichotokea nchini Somalia kitaandikwa kwenye ukurasa wa dhahabu katika historia ya nchi hiyo, na kwamba rais aliyemaliza muda wake Sheikh Sharif Ahmed atakumbukwa daima kwa mchango wake katika maendeleo. Mohamud aliezea matumaini yake kwa Somalia kuanza kuelekea katika maisha bora na kusahau matatizo yote iliyoyapitia.

Sheikh Sharif Ahmed akubali kushindwa
Kwa upande wake Sheikh Sharif alikbali kushindwa katika kura hiyo ambayo ni hatua ya mwisho katika mchakato huo ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa, uliolenga kuweka utawala mpya katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika. "Nampongeza ndugu yagu Hassan Mohamud kwa ushindi wake ambao ni wa haki na nimeridhishwa nao", alisema Sharif katika hotuba yake baada ya kutangazwa kwa matokeo na kuahidi kufanya kazi pamoja na rais mpya kama ambavyo angependa kufanya kazi na watu kama angeshinda.

Uchaguzi huo wa Jumatatu ni matokeo ya mpango wa amani ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa wa kukomesha mgogoro ambao umesababisha vifo vya maelfu ya Wasomali na kuwalaazimisha wengine kuyakimbia makaazi yao. Pamoja na hayo, bado wanamgambo wa al-Shabaab wanadhibiti maeneo mengi katikati na kusini mwa Somalia, wakati maharamia, watawala wa serikali za mitaa na makundi ya wanamgambo wanaoiunga mkono serikali yanapambana kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa katika nchi hiyo.

Mwanamke akipeperush bango lililokuwa na picha ya rais Sheikh Sharif Ahmed.

Mwanamke akipeperush bango lililokuwa na picha ya rais Sheikh Sharif Ahmed.

Changamoto zinazomkabili rais mpya
Kinachosubiriwa sasa ni kuona kama makundi yote yanayohasimiana nchini humo yataheshimu matokeo hayo, au yatajaribu kuvuruga serikali mpya. Bashir Ali Abdikadir, mwanafunzi wa Kisomali alisema rais mpya anapaswa kushughulikia suala la usalama kwanza, na kisha miundombinu ya kijamii, kuwarudisha wakimbizi na kuyakomboa maeneo mengine yanayodhibitiwa na wanamgambo wa al-Shabaab.

Mohamud pia atakabiliwa na changamoto ya sifa mbaya ya Somalia kama nchi inayoongiza kwa rushwa duniani. Mwezi Julai, kundi la Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia liliripoti kuwa liligundua kuwa kwa kila dola 10 za Marekani za mapato ya taifa kati ya mwaka 2009 na 2010, dola 7 hazikufika katika hazina ya serikali.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe,
Mhariri: Mohammed Khelef