1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Slovakia yachukua urais Umoja wa Ulaya

Sylvia Mwehozi1 Julai 2016

Slovakia inachukua urais wa Muungano wa Umoja wa Ulaya Ijumaa(01.07.2016), ikilenga kutumia nafasi hiyo kusaidia kuunganisha tena wananchi wake na Umoja huo na kurejesha uwezo wa maamuzi mikononi mwa mataifa ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/1JHM6
Frankreich Robert Fico in Paris
Picha: Reuters/S. Mahe

Akizungumzia mipango ya taifa lake kwa kipindi cha miezi sita ijayo, Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico amesema sera ya wahamiaji ya Umoja wa Ulaya imeshindwa kufanya kazi na kwamba Ulaya yenyewe imeshindwa kuwasiliana na wananchi wake.

Ameyataja mataifa makubwa katika Umoja huo, Ufaransa, Ujerumani na Italia, kuwa yameiendesha Ulaya kwa muda mrefu, na ni wakati sasa kwao kusikiliza nchi kama Slovakia ambayo imejiunga na Umoja huo tangu mwaka 2004.

Slovakia iliyojitenga na Jamhuri ya Czech mwaka 1993, ina wakaazi milioni 5.4, ikiwa ni asilimia 1 ya wakaazi wa Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu Fico amesema kuwa "uamuzi muhimu juu ya mustakabali wa Ulaya hauwezi kuwa wa mwanachama mmoja au wawili ama waanzilishi pekee." Fico ameongeza kwamba kamwe hawawezi kufanikiwa kwa kuwa na sera zisizofanya kazi.

Serikali ya Fico inakikosoa pia chombo kikubwa cha utendaji katika Umoja huo, Tume ya Ulaya, ambayo mamlaka yake yameongezeka tangu mkataba wa Lisbon wa mwaka 2009, kwa kuamuru utekelezwaji sera kutoka Brussels.

Waziri wa Mambo ya Nje Miroslav Lajcak anasema kwamba "zipo hisia miongoni mwa wanachama za kuona wanatengwa" akiongeza kuwa sera zinapaswa kuendeshwa na nchi wanachama na kazi ya Tume ni kuzigeuza kuwa sheria. Lajcak anasema mataifa ni lazima yawe na mamlaka zaidi kwa sababu "ni huko ndiko ambako wananchi wanaishi, hawaishi katika taasisi."

Angela Merkel na waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico
Angela Merkel na waziri mkuu wa Slovakia Robert FicoPicha: picture-alliance/dpa/J. Carstensen

Suala la wahamiaji lilionekana kama moja sababu kubwa iliyochochea uamuzi wa wiki iliyopita wa wapiga kura wa Uingereza wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Lakini wasiwasi wa Uingereza umejikita katika wahamiaji wanaotoka katika nchi nyingine za Ulaya na waingereza wenyewe kuona kama wanatumia faida ya ustawi wa taifa lao.

Mataifa mengine ndani ya Umoja huo yamechukizwa na sera ya wakimbizi. Mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya yanachukizwa na sera ya wakimbizi ya Umoja huo. Slovakia yenyewe pia ilikerwa na mpango wa lazima wa Tume ya Ulaya wa kugawana wakimbizi miongoni mwa nchi wanachama kutoka Iraq na Syria ambao wamemiminika na kuleta mzigo kwa Italia na Ugiriki.

Urais wa Umoja wa Ulaya huzunguka nchi wanachama kila baada ya miezi sita, na hivi karibuni ulikuwa mikononi mwa Uholanzi na ikaonekana kuweka vipaumbele katika ajenda za Umoja wa Ulaya na kufanyia kazi ya kumaliza tofauti na kufikia maafikiano.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Mohammed Khelef