1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sisi ndio Mayahudi wa karne ya 21 - Maduro

Mohammed Khelef
17 Mei 2017

Rais Nicolas Maduro amefaunanisha udhalilishaji wanaofanyiwa maafisa wa serikali yake na familia zao nje ya nchi hiyo na mateso waliyotendewa Mayahudi chini ya Wanazi, akiapa kuendelea kupambana.

https://p.dw.com/p/2d7x3
Venezuela Caracas Demonstrationen
Picha: Getty Images/AFP/C. Becerra

Maduro alisema kupitia televisheni hapo jana kwamba maandamano ya leo ya wapinzani mjini Caracas ni mabaki ya maandamano kama hayo wakati wa kuibuka kwa siasa za Kinazi na Ufashisti kabla ya Vita vya Pili vya Dunia barani Ulaya.

"Sisi ndiyo Mayahudi wapya wa karne ya 21 ambao Hitler aliwauwa," alisema Maduro wakati wa kikao cha baraza lake la mawaziri. "Hatuna nyota manjano ya Daudi... tuna nyoyo nyekundu ambazo zimejaa hamu ya kupambana kwa ajili ya heshima ya kibinaadamu. Na tutawashinda, Wanazi hawa wa karne ya 21."

Wanazi wa Kijerumani na washirika wao waliwauwa Mayahudi milioni sita kwenye mauaji ya maangamizi yaitwayo Holocaust katika miaka ya 1930 na 1940.

Kwa wiki kadhaa sasa, mitandao ya kijamii imekuwa ikirusha vidio za wahamiaji wa Venezuela kutoka Marekani hadi Australia wakiwamwagia matusi hadharani maafisa wa serikali na wakati mwengine hata familia zao.

Venezuela Erneut Proteste gegen die Regierung
Maandamano ya kumpinga Maduro yazidi kupata uungwaji mkonoPicha: Reuters/C. Garcia Rawlins

Wakosoaji wa Maduro wanasema ni jambo la aibu kwa maafisa hao wa serikali kutumia fedha za umma kutembea nje ya nchi, ilhali ndani ya nchi watu wanashindwa hata kupata mlo wao wa siku na huku watoto wakifa kwa kukosa matibabu.

Hata hivyo, waungaji mkono wa Maduro wanasema kuwashambulia maafisa wa serikali kwa matusi hadharani si njia sahihi ya kupambana na serikali. 

Wapinzani wa serikali, wanaomtuhumu Maduro kwa kuwa dikteta kwa kuahirisha uchaguzi na kutaka kuandika katiba upya, wamekuwa wakifanya maandamano takribani kila siku tangu mwezi Aprili. Zaidi ya watu 40 wameuawa kwenye maandamano hayo, ambayo wakati mwengine hugeuka kuwa ya fujo.

Kiongozi wa zamani wa Kisoshaliti nchini humo, Marehemu Hugo Chavez aliyekufa kwa saratani mwaka 2013, ambaye pia ndiye shujaa na mtangulizi wa Maduro, alikuwa akituhumiwa kutumia kauli zisiso maana kuhusiana na Mayahudi wakati wa utawala wake wa miaka 14. 

Mwenyewe Chavez alitupilia mbali tuhuma hizo akisema kuwa ni kampeni za makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia dhidi yake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf