1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bendera zapepea nusu mlingoti mjini Moscow

30 Machi 2010

Rais Medvedev na waziri mkuu, Putin waapa kukabiliana na ugaidi

https://p.dw.com/p/MhfU
Eneo la mripuko kwenye reli za treni, MoscowPicha: picture alliance / dpa

Raia mjini Moscow leo w siku maalum wanaomboleza vifo vya watu waliouwawa baada ya miripuko kwenye treni jana asubuhi. Wasafiri wameanza tena kutumia treni ingawa katika hali ya uoga. Taarifa zinasema sasa idadi ya watu waliouawa imefikia 39 baada ya mtu mwingine kufariki wakati akitibiwa hospitalini.

Bendera mjini Moscow zinapepea nusu mlingoti na Wakaazi wa Moscow wanaendelea kuweka shada za maua na kuwasha mishumaa katika maeneo yaliyokumbwa na miripuko inayotuhumiwa kupangwa na kundi la waasi wa kaskazini.

Trauer U-Bahn Anschlag Moskau ***no Flash***
Mrusi aomboleza katika eneo la mripuko, wakaazi waweka shada za maua na kuwasha mishumaaPicha: AP

Vyombo vya habari vimeripoti kwamba usalama unaimarishwa na maafisa wa polisi wamo katika vituo vya treni kuanzia mji wa St. Petersburg hadi Novosibirsk katika eneo la Siberia.

Vipindi vya burudani katika redio na televisheni mjini Moscow vimesimamishwa huku siku ya kuomboleza ikizingatiwa kuwakumbuka waliofariki katika miripuko mbaya zaidi kutokea katika kipindi cha miaka sita iliyopita na iliyotekelezwa na wanawake wawili wa kujitoa mhanga.

Wasafiri wa asubuhi waliingia katika treni kwa uoga hasa katika vituo vilivyoathirika vya Lubyanka na kingine karibu na bustani la utamaduni.

Katya Vankova mwanafunzi wa somo la biashara alisema akiwa kwenye treni alisikia saa ya abiria mwingine ikilia na alishtuka akifikiri ni sauti ya kuashiria sekunde kadhaa kabla bomu kuripuka.

Katika kituo karibu na bustani ya utamaduni mjini Moscow wakaazi waliweka mashada ya maua yenye tepe nyeupe na wengine kuweka alama zinazoashiri msalaba.

Rais wa urusi Dmitry Medevedev na Waziri wake mkuu Vladmir putin wameapa kukabiliana na kitisho cha ugaidi.

Russland Zahlreiche Tote bei U-Bahn-Explosionen in Moskau Dmitry Medwedew‎ Flash-Galerie
Rais Medvedev na viongozi wa Urusi waomboleza waliouawa.Picha: AP

Hakuna kundi lililojitokeza kutangaza kuhusika na miripuko hiyo lakini mkuu wa shirika la ujasusi la Urusi, Alexander Bortnikov amewatuhumu wanamgambo wa kaskazini waliokiri watashambulia miji ya Urusi na mabomba ya kusafirisha mafuta.

Ramzan Kayrov, kiongozi wa Wachechen anayeungwa mkono na uongozi wa Kremlin amesema washukiwa wanaowauwa raia wasiokuwa na hatia wanafaa kuuwawa kwa kuwekewa sumu kama panya.

Wakati huo huo Mawaziri wa nchi nane zilizoendelea kiviwanda zinazojulikana kama G8 wanaokutana mjini Ottawa, Canada kwa mkutano wa usalama, wamelaani miripuko ya jana mjini Moscow na metuma rambirambi zao kwa jamaa wa waathirika na watu wa Urusi kwa jumla.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters/AFP/DPA

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed