Siku ya kimataifa dhidi ya adhabu ya kifo | Masuala ya Jamii | DW | 10.10.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Siku ya kimataifa dhidi ya adhabu ya kifo

Tokea miaka mitano iliopita siku ya leo imekuwa ikuadhimishwa kuwa ni siku ya kimataifa dhidi ya adhabu ya kifo. Habari nzuri ya siku hii ni kwamba nchi 128 zimeondoa adhabu hii. Lakini habari mbaya ni kuwa bado kuna nchi 68 ambapo adhabu ya kifo inatumika.

Mhukumiwa wa adhabu ya kifo nchini China

Mhukumiwa wa adhabu ya kifo nchini China

Chama kilichoanzisha siku hii ni Muungano wa kimataifa wa kupambana na adhabu ya kifo, WCADP. Ni muungano wa zaidi ya mashirika 50 yasiyo ya kiserikali, jumuiya za wanasheria na jumuiya za wafanyakazi. Kwa kushirikiana, vyama hivi vinatumai kuyapa uzito malalamiko yao dhidi ya adhabu ya kifo. Kwa mujibu wa muungano huo, adhabu hiyo ni kinyume cha azimio la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Ibara ya tatu ya azimio hili inasema kuwa kila mtu ana haki ya kuishi. Na katika ibara ya tano inasemekana kuwa hairuhusiwi kuwatesa watu au kuwapa adhabu ya kinyama.

Nchi ambayo inakosolewa zaidi kwa matumizi yake ya adhabu ya kifo ni China. Kisheria kuna makosa 69 yanayoweza kuadhibiwa na kuuawa, kama vile mauaji, rushwa au kutolipa kodi. Mara kwa mara adhabu hiyo bado inatekelezwa hadharani.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la kupigania haki za binadamu, Amnesty International, katika mwaka 2005 watu 1770 walipewa adhabu ya kifo nchini Uchina. Hata hivyo, wataalamu wa kisheria wanakadiria idadi hii kuwa kubwa zaidi kufikia 8000 kwa vile mara nyingi kesi za adhabu ya kifo hazijulikani.

Mwaka huu maneno makuu ya siku hii ni: “Adhabu ya kifo – kama sheria zikishindwa”. Oliver Hendrich ambaye ni mhusika wa suala la adhabu ya kifo katika tawi la Ujerumani la Amnesty International, anaeleza zaidi kuhusu maneno haya: “Kwa kutumia maneno haya – sheria zikishindwa – tunataka kuweka wazi kwamba, juu ya kukosoa adhabu ya kifo kwa sababu za haki za binadamu, kuna matatizo mengi ya kisheria yanayotokea mara kwa mara. Hiyo ni sababu nyingine ya kuipinga adhabu ya kifo. Nitawapa mifano: ni kesi za mahakamani ambazo haziendeshwi sawa sawa, ni kuwahukumu kifo watu wasio na hatia, ni hukumu ya kifo dhidi ya vijana au dhidi ya watu wenye wazimu.”

Inajulikana kwa mfano kuwa watu kadhaa kati ya watu 1000 waliohukumiwa kifo nchini Marekani tangu adhabu ya kifo kutumika tena kuanzia mwaka 1976 walikuwa wenye wazimu. Vile vile inajulikana kwamba vijana kadhaa waliadhibiwa kunyongwa nchini Iran.

Kwa jumla idadi ya nchi zilizoondoa adhabu ya kifo inazidi kuongezeka. Mwaka huu, nchi ya Ufilippino ilifuta adhabu ya kifo. Bado lakini watu elfu kadhaa wanaadhibiwa kunyongwa kila mwaka, hasa katika nchi za China, Marekani, Iran na Saudi-Arabia.


 • Tarehe 10.10.2006
 • Mwandishi Helle Jeppesen / Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHmQ
 • Tarehe 10.10.2006
 • Mwandishi Helle Jeppesen / Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHmQ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com