Sigmar Gabriel azuru Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sigmar Gabriel azuru Marekani

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema atawasilisha ujumbe wa kirafiki nchini Marekani wakati atakapozuru nchini humo hii leo (02.02.2017)

Sigmar Gabriel atakua waziri wa kwanza wa mambo ya nje kukutana na waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ambaye alithibitishwa rasmi katika wadhifa hao hapo jana.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani  amesema  ziara yake hiyo inalenga kuwahakikishia washirika wao Marekani juu ya maslahi ya Ujerumani na kuwa anatarajia watakuwa na majadiliano mazuri na yaliyo wazi. 

Ziara ya Gabriel inakuja ikiwa ni siku mbili baada ya mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu katika ikulu ya White House ambaye anatarajiwa kuongoza baraza la biashara la ikulu ya White House Peter Navarro  kuishutumu Ujerumani kwa kutumia sarafu ya Euro kuikandamiza Marekani na washirika wake katika Umoja wa Ulaya.

Trump akosoa sera za Kansela Merkel kuhusiana na wahamiaji

USA Präsident Donald Trump Telefonat mit Australiens Premierminister Malcolm Turnbull (picture-alliance/dpa/Pete Marovich/CNP/AdMedia)

Rais wa Marekani Donald Trump

Rais  Donald Trump naye pia amemkosoa kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa sera yake ya kuweka milango wazi kwa wakimbizi huku pia Kansela Merkel akimshutumu Trump kwa kusaini agizo la kuwazuia wahamiaji kutoka mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia nchini Marekani.

Ilikuwa bado haijafahamika iwapo Sigmar Gabriel ambaye wiki iliyopita  aliteuliwa kushika wadhifa huo wa waziri wa mambo ya nje pamoja na majukumu yake mengine kama Naibu Kansela wa Ujerumani,  atakutana pia na Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence.  Hata hivyo Sigmar Gabriel hakupangiwa ratiba ya kukutana na Rais Donald Trump.

Sigmar Gabriel amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kufanya ziara hiyo mapema akisema Ujerumani ina maswali mengi kuhusiana na sera ya nje ya  sasa ya  Marekani.

Alisema kuna masuala muhimu katika ajenda ya kimataifa ambayo nchi hizo mbili pamoja na Ulaya kwa ujumla zinapaswa kushauriana kwa ukaribu zaidi ikiwa ni pamoja na ushiriki wa Marekani katika Jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi NATO.

Ujerumani tayari imeonekana kusitushwa na msimamo wa Donald Trump juu ya ushirikiano huo katika NATO. Hata hivyo serikali ya Ujerumani inatumaini kuwa waziri mpya wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson  pamoja na waziri mpya wa ulinzi wa nchi hiyo James Mattis watamshauri vizuri Rais Trump.

Wakati Waziri wa ulinzi James Mattis akiwa tayari ameonesha msimamo wake wa kuunga mkono ushirikiano wa NATO waziri wa mpya wa mambo ya nje wa Marekani Tillerson amekuwa akikosolewa kutokana na ushirikiano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakati waziri huyo alipokuwa mtendaji mkuu wa kampuni ya kimataifa ya mafuta na gesi ya Exxon Mobil.

Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE/ECA

Mhariri : Iddi Ssessanga

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com