1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa kuingilia uteuzi wa ICC

30 Mei 2011

Wakati Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ikijiandaa kuwachagua majaji sita na mwendesha mashtaka mpya, wachambuzi wanaonya siasa itatumika, badala ya sifa zinazostahiki, kuwatathmini watu hao katika nyadhifa hizo.

https://p.dw.com/p/11QsP
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Luis Moreno Ocampo
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Luis Moreno OcampoPicha: AP

Mchakato huo unaanza mwezi ujao (Juni 2011) wakati kura zikitazamiwa kupigwa mwezi wa Disemba. Lakini tayari kuna dalili kwamba nchi zilizosaini Mkataba wa Rome ulioanzisha mahakama hiyo zitaufanya mchakato huo kuwa wa kisiasa zaidi kuliko wa kitaaluma.

Katika mkutano wake wa kilele hapo mwezi wa Januari, Umoja wa Afrika ulidokeza kwamba utapigania kuchaguliwa kwa mwendesha mashtaka wa Afrika katika mahkama hiyo. Umoja huo ulitoa azimio lililotaja juu ya ushiriki muhimu wa Afrika katika mahkama hiyo, halikadhalika ukweli wa mambo kwamba hakuna nchi yoyote ya Afrika inayoongoza kitengo chochote kile kikuu cha taasisi hiyo.

Kesi zote ambazo tayari zinashughulikiwa hivi sasa na mahkama hiyo zinahusu uhalifu uliotendeka Afrika ukweli ambao umepelekea kuzuka shutuma dhidi ya mahkama hiyo kutoka wale wanaotaka kuipachika jina mahkama hiyo kuwa ni chombo kwa ajili ya maslahi ya mataifa ya magharibi.

Isitoshe Afrika inajigamba kwamba ina nchi nyingi zilizosaini sheria ya Rome kuliko bara lolote lile duniani.

Juu ya kwamba Umoja wa Afrika haukuonyesha dhahiri inataka kugombea wadhifa upi hasa na kuamua kulijadili suala hilo katika mkutano wake wa kilele uliopangwa kufanyika hapo tarehe 23 Juni, wachambuzi wanasema sio kitu cha siri kwamba chombo hicho kilikuwa kinataka Muafrika achukuwe nafasi ya mwendesha mashtaka wa hivi sasa Luis Moreno Ocampo.

"Ni wazi kwamba wangependelea sana mgombea wa Afrika." Anasema Param-Preet Singh mshauri mwandamizi wa Mpango wa Haki katika Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch la Marekani, ambalo limetowa wito kwa uchaguzi huo kufanyika kwa kuzingatia sifa za wagombea na kwamba asichaguliwe kwa sababu tu ametoka eneo fulani. Human Rights Watch imetaka hicho kisiwe kigezo.

William Pace, amabye ni msimamizi wa muungano kwa ajili ya Mahkama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu, ambalo ni kundi la zaidi ya mashirika 2,500 ya kiraia, amesema mojawapo ya hatari zinazoweza kuzuka kwa kutumia siasa katika uchaguzi huo wa mahkama ya ICC ni kwamba wanaweza kuigeuza kazi yenyewe halisi ya mahkama kuwa ya kisiasa.

Akitowa mfano katika uchaguzi wa mwendesha mashtaka, Pace anasema baadhi ya nchi zinaweza kumuunga mkono mgombea kwa sharti kwamba mgombea huyo anakubali kutofanya uchunguzi kwenye ardhi za nchi hizo.

Mojawapo ya wagombea waliotajwa kuwa wanaweza kuwa wagombea wa wadhifa wa mwendesha mashtaka waliopendekezwa na Umoja wa Afrika ni Fatou Bensouda wa Gambia, ambaye ni Naibu wa Ocampo na ambaye ana sifa za hali ya juu kustahiki wadhifa huo.

Kwa kuwa mgombea mkuu wa Afrika hadi hivi sasa inajitokeza kuwa ni mwanamke, watu wengi wamekuwa wakijiuliza iwapo jambo hilo ni sababu za ziada katika juhudi zinazofanyika hivi sasa kuuzuwiya Umoja wa Afrika kuidhinisha mgombea wao.

Mahkama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu imeunda kamati ya watu watano kutafuta mgombea na kuichuja orodha yake hadi kufikia wagombea watatu kuwania wadhifa huo wa mwendesha mashtaka. Wakati wa uchaguzi huo wa Desemba, Mkataba wa Rome unataja kwamba nchi 114 zinatakiwa zifikie muafaka wa mgombea na kushindwa kufanya hivyo inabidi ifanyike kura ya siri kumchagua mgombea.

Mbali ya kuchaguliwa kwa wajumbe wa kamati ya bajeti na fedha na wale wa kamati kuu hapo mwezi wa Desemba, chaguzi za rais wa mahkama hiyo na makamo wake wawili zitafanyika mapema mwaka 2012.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS
Mhariri: Bruce Amani