1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shule zote nchini Kenya kufunguliwa tena mwezi Januari

Thelma Mwadzaya16 Novemba 2020

Wakenya wanashusha pumzi baada ya tangazo kubainisha kuwa shule zote zitafunguliwa kikamilifu tarehe 4 Januari mwakani. Mitihani ya kitaifa pia itafanyika mwanzoni mwa mwaka kabla ya wanafunzi kusogea mbele darasani.

https://p.dw.com/p/3lMla
Kenia Nairobi | Corona | Wiedereröffnung der Schulen
Picha: Thomas Mukoya/Reuters

Shule zote zilifungwa rasmi miezi 8 iliyopita baada ya kisa cha kwanza cha COVID 19 kutangazwa rasmi. Wakati huo huo marufuku ya kutotoka nje usiku inafikia muda wake wa mwisho siku moja kabla ya shule zote kufunguliwa rasmi. 

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kikao na washika dau, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha aliweka bayana kuwa shule zote zitafunguliwa kikamilifu tarehe 4 mwezi wa Januari mwakani.

Kiasi ya wanafunzi milioni 10 wamekuwa nyumbani tangu mwanzoni mwa mwaka ili kuepuka maambukizi ya COVID 19.Wanafunzi wa darasa la 4 chini ya mfumo wa CBC waliokuwa wamerejea shuleni mwezi wa Oktoba mwaka huu wataenda likizo wakati wenzao watakuwa wanakamilisha masomo ya muhula wa tatu. Wanafunzi wengine nao pia wataruhusiwa kuchukua likizo watakapokamilisha muhula wa pili ifikapo tarehe 19 mwezi wa Machi mwakani. Dhamira ni kuipisha mitihani ya kitaifa ya darasa la nane KCPE na kidato cha nne, KCSE. Wakati huo huo afisa mkuu mtendaji wa tume ya kuwaajiri walimu nchini Kenya,TSC, Nancy Macharia anawarai walio na umri wa zaidi ya miaka 58 kusalia nyumbani.

Kenia Nairobi | Schulunterricht & Kenya Certificate of Primary Education
Wanafunzi wa shule ya msingi ya NairobiPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Bi Macharia aliweka bayana kuwa walimu hao hawatapigwa kalamu kwani ni agizo la rais na kuwa watatibiwa endapo wataambukizwa magonjwa yanayofungamana na COVID 19. Wanafunzi wa darasa la 4 ambao walirejea shuleni mwezi wa Oktoba wataingia darasa la tano mnamo Julai mwakani. Ijapokuwa waziri wa elimu wa Kenya Profesa George Magoha anashikilia kuwa shule ndio mahala salama zaidi kwa wanafunzi,wasiwasi umetanda miongoni mwa wazazi na walimu ukizingatia kuwa maambukizi ya corona yanaongezeka nchini Kenya.

Wiki iliyopita Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa masomo yote ya shule ya msingi yaanze tena upya ana kwa ana ifikapo januari mwakani. Wazazi wamekuwa na hisia mseto.

Shule zinazofuata mitaala ya kigeni nazo pia zitafunguliwa tarehe 4 Januari mwakani.