1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughuli ya kudhibitisha kura za Urais Zimbabwe yaanza

Mwakideu, Alex1 Mei 2008

Wanaharakati wa upinzani wakamatwa huku katibu mkuu wa chama cha MDC akitafutwa na polisi

https://p.dw.com/p/Drjn
Katibu wa chama cha upinzani MDC Tendai Biti anaetafutwa na polisiPicha: AP


Wakati tume ya uchaguzi ya Zimbabwe inaendelea na shghuli ya kudhibitisha matokeo ya uchaguzi wa Urais, wazimbabwe nao wanasubiri kuona mwelekeo mpya wa siasa nchini humo.


Wakati huo huo wanaharakati kumi wa chama cha upinzani Movement for Democratic Change wamekamatwa kwa mashtaka ya kuzua ghasia, kuteka watu nyara na kujaribu kuuwa.


Wawakilishi wa kiongozi wa chama cha upinzani Movement for Democratic Change na chama tawala ZANU PF wanakutana na tume ya uchaguzi ya Zimbabwe mjini Harare ili waweze kulinganisha hesabu za kura walizopiga na hesabu rasmi za tume hiyo.


Wakati huo huo katibu mkuu wa chama cha upinzani Tendai Biti anatafutwa na polisi kwa mashtaka ya kutangaza matokeo ya Urais na mapema; jambo ambalo mkuu wa polisi Augustine Chihuri anasema linachochea ghasia.


Biti amekuwa akiishi uhamishoni mwa wiki kadhaa sasa.


Mkutano wa kudhibitisha matokeo ya urais unafanyika baada ya duru kutoka tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kusema kwamba Tsvangirai anaongoza kwa wingi wa kura kati ya asilimia 47 na asilimia 50.


Siku zaidi ya mwezi zimepita na matokeo rasmi ya uchaguzi wa Urais hayajatangazwa. Hata hivyo matokeo hayo huenda yakatangazwa baada ya mkutano ulioanza leo ambao maafisa wa tume wanasema utachukua siku tatu.


Tsvangirai kiongozi mwenye miaka 56 alikuwa anashindani na Mugabe mwenye miaka 84 anayeonekana kama shujaa alieleta uhuru katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika na ambaye ameiongoza tangu wakati huo wa uhuru mwaka wa 1980.


Mapema Tsvangirai alijitangaza mshindi kulingana na hesabu za kura zilizopigwa na chama chake lakini upande wa Mugabe unasema uchaguzi huo unahitaji kurejelewa.


Alipoulizwa nini kitafanyika matokeo rasmi ya uchaguzi yatakapotofautiana na kura za wagombea mwenyekiti wa tume ya uchaguzi George Chiweshe alijibu kwa maneno machache kwamba wagombea hao lazima watakubali.


Tume ya uchaguzi na wawakilishi wa viongozi hao wamekataa kutabiri matokeo rasmi ya kura za urais. Waziri wa sheria Patrick Chinamasa anaemwakilisha Mugabe amesema mkutano huo ndio utakaoamua. Chris Mbanda anaemwakilisha Tsvangirai amesema shughuli hiyo inaweza kuchukua siku moja au mbili, inaweza kuchukua wiki au pia mwezi.


Mapema tume ya uchaguzi ilitangaza ushindi wa chama cha MDC katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika tarehe 29 sambamba na ule wa urais na mabaraza ya miji. Chama tawala cha ZANU PF kilikuwa hakijawahi kushindwa kwa wingi wa wabunge kwa miaka 28.


Mugabe anashutumiwa kwa utawala wa kidikteta na kuzorotesha uchumi wa Zimbabwe kwa sera yake ya mwaka wa 2000 iliyopelekea kuwafukuzwa kwa wazungu katika mashamba yao kwa kutumia nguvu.


Hatahivyo serikali yake inalaumu Umoja wa Ulaya na Marekani kwa kuiwekea vikwazo ambavyo vimesababisha matatizo hayo ya ukosefu wa kazi wa asilimia 80 na mfumuko wa bei wa asilimia laki moja na sitini na tano.


Wakati huo huo wanaharakati kumi wa chama cha upinzani wamekatwa na polisi mjini Harare na Bindura kwa mashtaka ya utekaji nyara, kuzua ghasiana kujaribu kuuwa.


Msemaji wa polisi Andrew Phiri amesema wamewakata watu wanne wanaodaiwa kumteka nyara mwanajeshi mmoja mjini Bindura na wengine sita Harare kwa kuchoma basi.


Polisi wanaendelea kuchunguza visa hivyo na watuhumiwa kadhaa tayari wamefikishwa mahakamani.


Phiri anasema watuhumiwa wanne waliokamatwa mjini Bindura walikuwa wanaendesha gari lao walipomteka nyara mwanajeshi na kumtia ndani ya gari kabla ya kuelekea katika maeneo yasiojulikana.


Mwanajeshi mwenyewe alimudu kuruka nje ya gari hilo na anaendelea kutibiwa majeraha aliyopata.


Wafuasi takriban 30 wa upinzani akiwemo mkurugenzi wa chama cha MDC Luke Tamborinyoka na mwanahabari asiekuwa na mipaka wamekamatwa tangu uchaguzi wa machi 29 na wamewekwa rumande kwa mashtaka ya kuchoma gari katika siku ya kwanza ya mgomo uliopangwa na upinzani ili kushinikiza matokeo ya uchaguzi wa Urais.