Shirika la utangazaji Ugiriki lafungwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Shirika la utangazaji Ugiriki lafungwa

Serikali ya Ugiriki hapo jimetangaza kulifunga shirika la utangazaji la umma ERT ambalo limekuwa likiendesha shughuli za uanahabari kwa miaka 75 ili kubana matumizi,hatua ambayo imewashitusha wengi nchini humo

Vyama vya kisiasa na vyama vya wafanyikazi nchini humo vinajaribu kubatilisha uamuzi huo wa serikali wa kufunga vituo vya televisheni na redio vya ERT ili kutimiza masharti ya kukaza mkwiji katika juhudi za kujikwamua kutoka mgogoro wa kiuchumi.

Mitambo ya kupeperushia matangazo ya shirika hilo yalizimwa jana usiku katika hatua ambayo haikutarajiwa na wafanyakazi na wananchi wa Ugiriki katika kile msemaji wa serikali Simos Kedikoglou alichokitaja ubadhirifu na ukosefu wa uwazi kuwa sababu ya kufungwa kwake.

Kiongozi wa upinzani Alexis Tsipras amesema atamuomba Rais Carolos Papoulias leo kutotia saini agizo hilo la kufungwa kwa shirika hilo la umma kwani ajira za karibu wafanyikazi 2,7000 wa shirika hilo zitapotea.Tsipras ameitaja hatua hiyo kuwa mapinduzi ya nchi.

Maelfu ya raia nje ya majengo ya ERT

Maelfu ya raia nje ya majengo ya ERT

Maelfu ya raia walikusanyika katika makao makuu ya shirika hilo leo mjini Athens kuonyesha kuwaunga mkono wanahabari wa ERT ambao wamekataa kuondoka afisini mwao na wameendelea kupeperusha matangazo yao sasa kupitia mitandao huku wanahabari wa mashirika mengine nchini humo wakifanya migomo kupinga hatua hiyo ya serikali.

Vituo vya kibinafsi vyagoma kuunga ERT

Mkuu wa chama cha waandishi habari cha Ugiriki Dimitris Trimis amesema vituo vya televisheni,redio na magazeti nchini humo vimesitisha kazi na vinashiriki kwa mgomo ili kuwaunga mkono wenzao wa ERT.Mgomo huo umesababisha kukatishwa kabisa kwa matangazo kote nchini humo.

Mkurugenzi mkuu mtendaji wa ERT Emilios Latsios amesema wafanyakazi wametakiwa kuondoka kutoka majengo ya shirika hilo au wakamatwe lakini bado polisi hawajajaribu kuwaondoa wanahabari hao.

Serikali imesema ERT itafungwa kwa muda na itafunguliwa chini ya muundo tofauti na kuwaajiri wafanyikazi wachache tu.Na kwamba wafanyikazi wa sasa wote 2,655 wamefutwa kazi, watalipwa fidia na wataruhisiwa kutuma maombi ya kazi upya wakati litafunguliwa tena baadaye.

Rais wa chama cha wanahabari Ugiriki Dimittris Trimis

Rais wa chama cha wanahabari Ugiriki Dimittris Trimis

Ugiriki imekuwa ikichukua hatua ngumu katika siku za hivi karibuni ili kupunguza matumizi ya bajeti yake kuambatana na masharti ya wakopeshaji wake wa kimataifa.Serikali ilitangaza kuwa itawafuta kazi wafanyikazi 4,000 katika sekta ya umma mwaka huu na wengine 11,000 mwaka ujao ili kupata mikopo ya uokozi.

Siku ya jumatatu wawakilishi wa Umoja wa ulaya,shirika la fedha duniani na benki kuu ya ulaya walianza shughuli za uhasibu kutathimini hatua ambazo zimepigwa na nchi hiyo katika kutekeleza mpango wake wa kukaza mkwiji na kufanya mabadiliko ya kiuchumi ambayo ni pamoja na kupunguza sekta ya umma na kuzijumuisha au kuyafunga mashirika ya umma.

Mwandishi;Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com