1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria ya ushirikishaji wakimbizi yaafikiwa Ujerumani

Iddi14 Aprili 2016

Serikali ya Ujerumani imekubaliana juu ya mpango wa kuwashirikisha wakimbizi ndani ya jamii na kupambana na ugaidi. Kulingana na hatua hizo, wakimbizi wanaoshindwa kutimiza vigezo wanaweza kukatiwa msaada wa hifadhi.

https://p.dw.com/p/1IVCe
Kansela Angela Merkel (kulia), naibu wake Sigmar Gabriel (Kati) na mwenyekiti wa CSU Horst Seehorfer wakiwa kwenye mkutano wao mjini Berlin.
Kansela Angela Merkel (kulia), naibu wake Sigmar Gabriel (Kati) na mwenyekiti wa CSU Horst Seehorfer wakiwa kwenye mkutano wao mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Vyama vinavyotawala vya Christian Democratic Union CDU, Christian Social Union CSU na Social Demoractic Party SPD, vimesifu muswada mpya wa sheria ya ushirikishwaji wakimbizi uliyokubaliwa mapema leo, baada ya mkutano uliyodumu kwa saa saba mjini Berlin.

Vyama hivyo vimetangaza mipango ya kuamua kuhusu kanuni zao za kuunga mkono pamoja na changamoto, wakati wa mkutano wa faragha utakaofanyika mjini Meseberg Mei 24. Sheria hiyo inajumlisha orodha ya vikwazo kwa watafuta hifadhi wanaokataa kuchukuwa hatua za kushiriki ndani ya jamii ya Ujerumani.

"Miaka 50 tangu kuanza kwa uhamiaji, Ujerumani sasa imepata sheria mpya ya ushirikishwaji," aliandika kiongozi wa kundi la wabunge wa SPD katika bunge la Ujerumani - Bundestag - Thomasa Oppermann kwenye ukurasa wake wa Twitter baada ya kufikiwa kwa makubaliano baina ya vyama tawala.

Masharti ya hifadhi

Sheria hiyo ya ushirikishwaji inahusu hasa mipango yenye utata iliyopendekezwa na waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas die Maiziere, ya kuwanyima vibali vya ukaazi wa kudumu wakimbizi wasioonyesha juhudi za kutosha kujumuika katika jamii, ikiwemo kujifunza lugha ya Kijerumani.

Ili wakimbizi waweze kukabiliwa kuishi Ujerumani, laazima wachukuwe hatua kujishirikisha ndani ya jamii.
Ili wakimbizi waweze kukabiliwa kuishi Ujerumani, laazima wachukuwe hatua kujishirikisha ndani ya jamii.Picha: DW/N. Niebergall

Hatua hizo zitajaribu kuwapeleka haraka zaidi wakimbizi, ambao wengi wao wamekimbia vita nchini Syria, katika soko la ajira, kwa kusitishwa kwa muda wa miaka mitatu, hatua zinazozuwia kuajiriwa kwa raia wasiotoka Ulaya katika nafasi ambazo raia wa Ujerumani au wa Umoja wa Ulaya wana vigezo vya kuzijaza.

Mpango huo unanuwia kuunda ajira 100,000 za euro moja, ambamo wakimbizi wanaweza kufanya kazi kwa ujira wa kati ya euro moja na 2 na centi 50, bila mapato yao kuhesabiwa kwenye msaada wa ukimbizi.

Upinzani wakosoa

Lakini mwenyekiti wa chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto Die Linke Katja Kipping amelalamika akisema muungano unaotawala umeshindwa kufikia makubaliano ya mwisho kuhusu sera ya soko la ajira na masuala ya kijamii.

''Ni wazi kwamba hakuna makubaliano ya wazi juu ya kuzuwia ukijukaji katika ajira za muda na mikataba ya kazi na pia katika mifumo mikubwa ya ugawanyaji kama kodi ya mali zinazohamishika.

Kifupi ni kwamba hii serikali ya muungano haiko tayari kukabiliana na changamoto halisi za kijamii,'' alisema Kipping alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo.

Mwenyekiti wa chama cha upinzani Die Linke Katja Kipping anasema vyama tawala vimeshindwa kushughulikia changamoto ya halisi za kijamii.
Mwenyekiti wa chama cha upinzani Die Linke Katja Kipping anasema vyama tawala vimeshindwa kushughulikia changamoto ya halisi za kijamii.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Viongozi wa sekta ya biashara wametoa rai kuwa wakimbizi wanaweza kuwa na manufaa kwa uchumi wa Ujerumani katika kipindi cha muda mrefu, lakini idadi ya wanaowasili imepungua.

Kuimarisha mapambano dhidi ya ugaidi

Sheria hiyo pamoja na mpangokazi wake vinalenga pia kuimarisha rasilimali za ufadhili wa vikosi vya usalama vya taifa. Wanachama wa muungano unaoongoza pia wamekubaliana juu ya hatua za kuziwezesha idara za ujasusi za Ujerumani kubadilishana taarifa na washirika wa siri wa kigeni.

Hatua hiyo inajumlisha ubadilishanaji wa taarifa na idara washirika barani Ulaya, na pia nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami NATO pamoja na Israel.

Kansela Angela Merkel aliongoza mkutano huo, ambao ulihudhuriwa na mawaziri husika kutoka vyama vinavyounda muungano mkuu, na vile vile mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union Horst Seehofer.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, DW
Mhariri: Grace Patricia Kabogo