1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi yanataka utumizi wa sheria za dini ya kiisilamu

Faiz Musa27 Mei 2019

Makundi ya waisilamu wenye misimamo mikali nchini Sudan wanaliunga mkono jeshi la taifa katika kuhakikisha utumiaji wa sheria za dini ya kiisilamu katika taifa hilo zinasalia.

https://p.dw.com/p/3JCrj
Ramadan Islam Religion
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Huku mazungumzo baina ya viongozi wa waandamanji na jeshi la Sudan juu ya kutengeza baraza la mpito linalojumuisha raia yakisitishwa kwa muda, mamia ya wafuasi wa vyama vya kiisilamu katika siku za hivi karibuni wamekuwa katika mji mkuu wakionya kwamba hawatokubali makubaliano ambayo yataitenga sheria ya dini katika uongozi wa taifa hilo.

Vyama vya kiisilamu vilijiweka kando wakati kulikuwa na maandamano ya kumtoa Omar Al Bashir na hadi sasa vyama hivyo havijajiunga katika mvutano wa raia na jeshi katika kutengeneza baraza la mpito litakaloiendesha nchi hiyo kwa muda wa miaka mitatu. Lakini wanaunga mkono matakwa ya jeshi ya kutaka baraza hilo la mpito kuungozwa na mwanajeshi kinyume cha waandamanaji wanaotaka uongozi wa raia.

Kaimu kiongozi wa vuguvugu la waisilamu wanaotaka mageuzi ya haraka Hassan Rizk amesema wanakubaliana na waandamaji kwamba kuwepo na baraza la mawaziri ambao ni wataalamu ila wao wanataka baraza la mpito kuongozwa na mwanajeshi kwa sababi kuna tatizo la usalama.

Sudan Proteste in Khartum
Waandamanaji wakifuturu nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Hatibu mwenye msimamo mkali Abdelhay Yousef amekuwa akiongoza umati wa watu katika hotuba zake akipigia debe uongozi wa sheria ya kiisilamu  katika wilaya ya Jabra. Mwanachama katika muungano wa sheria ya dini wa Nusrat al-Sharia, Qasim Mursal amesema haitawezekana kubadili sera ya Sudan ya kutumia mfumo wa sheria huku kundi hilo likiongeza kwamba vikao baina ya waandamani na jeshi vimekuwa vikitenga vyama vya kiisilamu na vyama vyengine vya kisiasa.

"Ujumbe kwa miungano ya ukombozi na mabadiliko ni kwamba watu hawa wanajukumu nchini Sudan, na watu hawa wana usemi nchini Sudan, na ujumbe wetu kwa baraza la mpito la kijeshi ni kwamba watu hawa hawatauwacha utambulisho wao na kwamba mabadiliko Sudan yatasalia kuwa ya kiisilamu na kwamba bendera ya Uisilamu itaendelea kupepea nchini Sudan," asliema Qasim.

Vyama vya kiisilamu vilimuunga mkono Bashir

Naye mkuu wa muungano wa vyama vya kihafidhina, Tayeb Mustafa aliye pia rafiki wa muda mrefu wa aliyekuwa rais Omar Al Bashir, amesema vyama vya kiisilamu vimekuwa vikipinga mpango wa mpito kwa sababu ulikuwa unapuuza sheria ya kiisilamu. Wachambuzi wanasema vyama vya kiisilamu vilivyokuwa na ukaribu na Bashir hivi sasa vinapata wakati mgumu wa kujiunga na mavuguvugu ya makundi ya mabadiliko.

Mwanahabari maarufu Sudan Khaled Tijani anasema haiwezekani kuwa sawa chama ambacho kimekuwa kikipinga uongozi wa Bashiri na chama ambacho kilikuwa ndani ya uongozi wa Bashir hadi mwisho wa utawala wake.

Bashir aliingia madarakani kupitia mapinduzi yaliyoungwa mkono na vyama vya kiisilamu na tangu wakati huo bunge limekuwa likizingatia sheria ya dini ya kiisilamu katika kuweka sheria za nchi. Ila hadi sasa waandamanaji wamelinyamazia swala la iwapo sheria ya dini iko na nafasi katika mustakabali wa Sudan.

Siku ya Ijumaa mabasi yaliwabeba wafuasi wa vyama vya kiisilamu na kuwapeleka katika uwanja wa ikulu ya rais mjini Khartoum ambapo waliweza kufungua saum zao mwendo wa magharib na kuanza kupigia debe mpango wa sheria ya dini. Makundi hayo yalikuwa yakipaza sauti wakisema mapinduzi huru hayatakubali kuongozwa na makundi ya mrengo wa kushoto.

(AFPE)