Sheria kali zatowesha ndoto za maendeleo kwa wanawake wa Iraq. | Masuala ya Jamii | DW | 06.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Sheria kali zatowesha ndoto za maendeleo kwa wanawake wa Iraq.

Wakati mmoja mwanamke alikuwa na haki zaidi na uhuru nchini Iraq, kuliko mahala kwengine kokote katika kiarabu. sasa hali ni kinyume na ndoto ya mwanamke hasa katika elimu na nafasi ya kujiendeleza imeanza kutoweka.

Wanawake nchini Iraq, ambao ndoto za kujiendeleza hasa katika elimu imetoweka.

Wanawake nchini Iraq, ambao ndoto za kujiendeleza hasa katika elimu imetoweka.

Aliyekuwa kiongozi wa kidikteta nchini humo Saddam Hussein, aliendeleza elimu ya jamii, ambapo katika utawala wake, ilikuwa kawaida kwa mwanamke kushika nafasi za kazi kama profesa, dokta na afisa wa serikali, lakini leo wanawake wa Iraq wamekuwa wakiuawa na vikundi vya wanamgambo kwa kutofuata sheria kali za kiislamu.

Mkuu wa Polisi wa mji wa Basra Jalil Hannon mwezi Desemba aliwaambia waandishi wa Habari kwamba katika mji huo pekee kiasi cha wanawake 40, waliuawa katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Ameongeza kusema kuwa pia wana uhakika kwamba wapo wengine pia waliouawa ambao familia zao hazikutoa taarifa.

Wanamgambo wanaomilikiwa na chama cha Badr cha madhehebu ya Shia na jeshi la Mehd wanaongoza juhudi za kutekeleza sheria kali za kiislamu.

Serikali ya Iraq inayodhibitiwa na Washia imeonekana kama kuridhia kimya kimya hali hiyo na wakati mwingine moja kwa moja kuwaunga mkono.

Wakazi wa mji wa Basra na Baghdad waliliambia Shirika la Habari la IPS katika miezi ya hivi karibuni, kwamba wanawake ambao hawavai Hijab wamekuwa ni walengwa wakubwa wa mashambulio ya wanamgambo hao na kwamba wanawake wengi wanasema kuwa wamekuwa wakipewa vitisho vya kuuawa iwapo hawatatii.

Mwanafunzi mmoja wa kike ambaye alikimbia mji wa Basra na kuelekea Baghdad Zuhra Alwan anasema wanamgambo hao huwalazimisha kuvaa Hijab na kuacha kujipodoa.

Naye Mtafiti wa masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Baghdad, Mazin Abdul Jabbar anasema hali pia katika mji wa Baghdad sio tofauti, anafahamisha kuwa vyuo vikuu vyote vinadhibitiwa na wanamgambo wa kiislamu ambao wamekuwa wakiwabughudhi wanafunzi wa kike wakati wote na masharti ya kidini.

Anaseha hali hiyo imesababisha familia nyingi kuacha kuwapeleka mabinti zao katika shule za juu na vyuo.

Mapema mwaka 2007 Wizara ya Elimu ya Iraq, iligundua kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wasichana na wanawake wanaosoma hawahudhuri tena shuleni ama vyuoni.

Wanawake kadhaa walianza kutuhumiwa na masuala hayo kabla ya kutekwa, na kwamba wengi ya waliotekwa walikutwa wamekufa baadaye, na kwamba miili ya wengi ilikutwa katika majaa ya taka, huku ikionesha dalili za kubakwa na kuteswa.

Matatizo kama hayo pia yanawakuta wanawake wa mji wa Baquba mji mkuu wa jimbo la Diyala kilomita 40 kusini mashariki mwa mji wa Baghdad.

Wapo pia wanawake waliouawa kutokana na kazi zao na kwamba wapo waliobadili kazi zao kutokana na kuogopa hali hiyo.

Maisha ya wanawake yamebadilika na sasa wanaogopa kuvaa chochote bali nguo zenye kuwahifadhi zaidi, na uvaaji wa nguo za kisasa ni kama una halalisha kifo chako.

Kutokana na hali hiyo wanawake nchini humo wamejikuta wakiishi maisha ya upweke na kuwa katika hali ya kufadhaishwa, kwani wamekuwa hawana pa kwenda kwa ajili ya kujiliwaza na muda wao wamekuwea wakiutumia nyumbani tu, kama anavyothibitisha Um Ali mwanamke aliyeolewa katika mji wa Baquba, ambaye anasema sehemu anayoweza kwenda ni kwa wazazi wake tu na kwamba hana malengo yoyote ikiwemo elimu.

Katika eneo la kaskazini mwa Iraq linalodhibitiwa na Wakurd, wanawake 27 wa Kikurd waliuawa kutokana na kuhisiwa kuwa na mahusiano yasiyo halali katika kipindi cha miezi minne iliyopita.

Huku serikali ya Iraq ikiwa haina nguvu na ukereketwa wa dini ukiongezeka inaonekana hali za wanawake wa Iraq zinazidi kuwa mbaya.


 • Tarehe 06.03.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DJog
 • Tarehe 06.03.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DJog
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com