1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mukwege, Murad wakabidhiwa tuzo ya Nobel

Oumilkheir Hamidou
10 Desemba 2018

Tabibu wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Denis Mukwenge na Nadia Murad, msichana wa jamii ya Yazid aliyegeuzwa mtumwa wa kingono na wafuasi wa itikadi kali wa Dola la kiislam wamekabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel

https://p.dw.com/p/39oiy
Verleihung Friedensnobelpreis Denis Mukwege Nadia Murad
Picha: AFP/Getty Images/T. Schwarz

Katika  sherehe za kusisimua zilizohudhuriwa na familia ya kifalme na wageni mia kadhaa wa hishma, mwenyekiti wa kamati ya Nobel, bibi Berit Reiss-Anderssen amewasifu washindi hao wawili, Nadia Murad mwenye umri wa miaka 25 na tabiibu Denis Mukwege mwenye umri wa miaka 63 na kuwataja kuwa "Sauti yenye nguvu ya dunia katika ulimwengu wa leo."Mapambano ya kuania haki yamewaleta pamoja licha ya maeneo tofauti walikotokea.

Bibi Berit Reiss-Andersen ameendelea kusema:"Washindi wote wawili wanataka maovu yaandamwe kisheria, uhalifu wa vita lazma uadhibiwe na kwamba jukumu lisalie mabegani mwa jumuia ya kimataifa. Wote wawili wanastahiki kikamilifu tuzo ya amani ya Nobel."

Daktari Denis Mukwege akitoa shukurani kwa kutunukiwa tuzo ya amani ya Nobel
Daktari Denis Mukwege akitoa shukurani kwa kutunukiwa tuzo ya amani ya NobelPicha: NTB Scanpix/Haakon Mosvold Larsen/Reuters

Jumuia ya kimataifa inabidi iwe macho

Akitoa shukurani zake, daktari huyo wa maradhi ya wanawake Denis Mukwege amesema vita pekee vinabidi viwe vita dhidi ya hali ya watu  kutojali" na kuitolea wito jumuia ya kimataifa wasiyafumbie macho matumizi ya nguvu ya kingono katika maeneo ya mizozo.

Mukwege ambae juhudi zake katika eneo la mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo zimempatia sifa za shujaa anaepambana na ubakaji kama silaha ya vita ameitolea wito jumuia ya kimataifa ijiunge nao katika kukomesha madhila yanayoutia aibu ubinaadamu.

Nadia Murad-mwanaharakati wa kikurd aliyegeuzwa mtumwa wa kingono na wafuasi wa itikadi kali nchini Iraq
Nadia Murad-mwanaharakati wa kikurd aliyegeuzwa mtumwa wa kingono na wafuasi wa itikadi kali nchini IraqPicha: AFP/Getty Images/T. Schwarz

Ulinzi wa wayazid ni jukumu la jumuia ya kimataifa

Kwa upande wake Nadia Murad akishangiriwa miongononi mwa wengineo na  mwanaharakati wa haki za binaadam, muingereza mwenye asili ya Libnan, Amal Clooney amewasihi walimwengu wailinde jamii yake ya Yazid."Ulinzi wa wayazid ni jukumu la jumuia ya kimataifa na taasisi za kimataifa" amesema na kusisitiza "bila ya ulinzi wa kimataifa, hakuna kitakachowahakikishia kama hawatokabiliawa tena na balaa la mauwaji kutoka makundi mengine ya kigaidi".

Mbali na tuzo ya amani ya Nobel, tuzo nyengine za Nobel zimetolewa leo hii pia lakini mjini Stockholm, isipokuwa ile ya fasihi iliyoakhirishwa hadi mwaka 2019. Tuzo ya amani ya Nobel ni mchanganyiko wa nishani ya dhahabu, shahada na hundi ya safaru ya Sweeden  Crone milioni tisa ambayo ni sawa na Euro 871.000-

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/

Mhariri:Yusuf Saumu