Shauku ya kumuona Papa yaendelea | Masuala ya Jamii | DW | 23.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Shauku ya kumuona Papa yaendelea

Siku chache kabla ya kuwasili kwa kiongozi wa kanisa katoliki nchini Uganda,waumini na wafanyibiashara wana kila la kutabasamu

Huku shauku ya kumuona papa huyo ikiendelea ,picha za papa huyo na zile za rais Yoweri Msevevi zinauzwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala.

Kwenye duka la Jude colour solutions,duka linalouza bidhaa mbalimbali hivi sasa linauza baadhi ya vitu ambavyo vimechorwa picha ya kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani na picha ya rais Museveni.

Meneja wa duka la kanisa katoliki Bernard Ssenyondo mwenye umri wa miaka 32 anasema anafuraha kufuatia ziara hiyo inayotarajiwa nchini humo tarehe 27 na29 mwezi huu.

Ssenyondo amesema Papa Francis atakuwa kiongozi wa pili wa kanisa katoliki duniani ambaye yeye atamuona baada ya ziara ya Papa John Paul wa pili mwaka 1993 iliyofanyika alipokuwa shule ya msingi.

Kwenye rafu ya juu kwenye duka hilo kuna kombe alilopokea Ssenyondo kwa kuwa muwekaji chapa bora, mchapishaji na mfanyibiashara bora wa kutangaza bidhaa nchini Uganda,karibu na kombe hilo kuna bilauri la kuweka maua lenye picha ya papa Francis.

Biashara kuimarika

Symbolbild Katholische Kirche in Afrika

waumini wa kanisa katoliki wakiomba wakati wa misa

Ssenyondo anasema wanapata fedha kutokana na biashara hii tangu kampuni yake ilipoanza kuchapisha maelfu ya vifaa vya funguo,vikombe vikubwa,Shati na bidhaa nyingine mapema mwezi huu,baada ya kuteuliwa na kanisa katoliki nchini humo kuwa msambazaji rasmi wa bidhaa za mapambo.

Anasema anapata kufahamika kimataifa na sekta ya utalii itapokea fedha zaidi.

Uganda ni nchi ya pili kati ya mataifa matatu ya Afrika ambayo Papa atazuru,baada ya kufanya ziara ya siku mbili katika nchi jirani ya Kenya.

Kenya pia inaendelea kufanya maandalizi ya ziara hiyo ya Papa,kwa kusafisha mitaa yake,kuchonga miti huku mabango makubwa yakitundikwa kumkaribisha Papa huyo.

Askofu Alfred Rotich ambaye anaongoza kamati ya Kanisa Katoliki inayohusika na maandalizi ya ziara ya Papa,amesema wanajiandaa kwa waumini milioni moja watakaohudhuria.

Baada ya ziara ya siku mbili nchini Uganda,atasafiri kuelekea Jamhuri ya Afrika ya kati ambapo ziara yake itamalizika tarehe 30 mwezi Novemba kulingana na ratiba kuhusu ziara ya Papa Francis kutoka Vatican.

usalama wapewa umuhimu

Mataifa hayo matatu ambayo yana waumini wengi wakatoliki barani Afrika yamekumbwa na mizozo na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, na kusababisha usalama kuangaziwa kwenye ziara hiyo ya Papa.

Wanajeshi wa Kenya na Uganda wanapigana na kundi linalofungamana na mtandao wa Al Qaeda ,Al shabab nchini Somalia na magaidi hao wametekeleza msururu wa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Mashambulizi haya ni pamoja na yale ya mwaka 2010 mjini Kampala ambapo watu 76 waliuawa na ya nchini Kenya kundi hilo lilishambulia chuo kikuu cha Garissa na kusababisha vifo vya watu 148 na huku pia likivamia maduka ya Westgate mjini Nairobi ambapo watu 67 walifariki.

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati Catherine Samba Panza amesema anatumaini Papa ataendelea na ziara yake nchini humo mwezi huu licha ya nchi hiyo kukumbwa na mapigano na kuzua taharuki ya usalama.

Nchini Uganda karibu asilimia 40 ya watu ni wakatoliki.

"Papa Francis ni mnyenyekevu"amesema John Paul Guminkiriza,mwenye umri wa miaka 25 aliyepokea jina hilo baada ya ziara ya hapo nyuma ya Papa nchini humo.

Mwandishi:Bernard Maranga
Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com