1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sharapova, Serena wabanduliwa nje ya Australian Open

20 Januari 2014

Kinyang'anyiro cha Australian Open kinaendelea kusababisha mshangano kwa magwiji wa Tennis. Maria Sharapova amejiunga na kigogo mwenzake Serena Williams kwa kuondolewa katika duru ya nne ya dimba hilo.

https://p.dw.com/p/1AtsF
Australian Open 2014 Maria Scharapowa
Picha: Reuters

Rafael Nadal na bingwa wa Wimbledon Andy Murray walikabiliwa na kibarua kigumu kabla ya kufuzu katika robo fainali ya kinyang'anyiro hicho. Bingwa mara mbili Viktoria Azarenka sasa ndiye anayepigiwa upatu wa kufuzu katika fainali kwa upande wa wanawake, baada ya kumbandua nje Mmarekani Sloane Stephens. Sharapova aliduwazwa na Dominika Cibulkova.

Nadal alishinda seti tatu ngumu dhidi ya Kei Nishikori, wakati Murray akitokwa kijasho na kumshinda Mfaransa Stephane Robert. Bingwa mara nne wa Australian Open Roger Federer amempiku Jo Wilfried Tsonga, ambapo sasa atakuana na Murray katika robo fainali. Naye Nadal atashuka dimbani na Grigor Dimitrov. Azarenka atapambana na Agnieszka Radwanska au Mhispania Garbine Muguruza katika robo fainali.

Hapo kesho, mchezo wa kwanza wa robo fainali utaanza wakati Ivanovic atakapokutana na Eugenie Bouchard wakati naye Li Na akiangushana Flavia Pennetta. Katika upande wa wanaume, bingwa mtetezi mara tatu Novak Djokovic atacheza na Stanislas Wawrinka wakati naye David Ferrer akipambana na Tomas Berdych.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman