Shangwe zatawala Marekani na dunia kwa jumla baada ya Obama kuingia rasmi madarakani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 21.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Shangwe zatawala Marekani na dunia kwa jumla baada ya Obama kuingia rasmi madarakani

Viongozi mbali mbali wampongeza rais mpya

default

''Rais mpya Barack Hussein Obama na mkewe Michelle''

Barack Hussein Obama akila Kiapo kuwa rais wa 44 wa Marekani hapo jana jioni saa za Afrika Mashariki.

Obama aliapishwa rasmi kuingia madarakani na mwanasheria mkuu wa mahakama kuu ya Marekani John Roberts katika sherehe iliyohudhuriwa na zaidi ya watu millioni mbili waliomiminika katika viwanja vilivyo karibu na bunge mjini Washington Dc na mamilioni ya wengine duniani kote wakikusanyika kuangalia tukio hilo lililokuwa na msisimko mkubwa.

Maelfu ya watu nchini Marekani walioshuhudia tukio hilo kupitia televisheni kubwa zilizokuwa zimewekwa kila kona ya katika viwanja vya karibu na bunge walianza kupiga kelele na kunung'unika baada ya mwanasheria mkuu John Roberts kumuongoza vibaya kula kiapo Barack Obama ambapo ilimbidi rais huyo mpya kusitasita kidogo kabla ya mwanasheria mkuu kurudia tena kifungu cha pili cha kiapo.

Shangwe na nderemo zilitawala kila pembe sio tu Marekani bali duniani kote kuanzia barani Afrika,mashariki ya kati hadi mashariki ya mbali.Wazee kwa vijana,wake kwa waume,weusi na weupe hakuna aliyebakia nyuma.Kulikuwa na usalama wa hali ya juu kote.Katika Hotuba yake ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na wengi Obama aligusia mengi kuanzia hali ngumu ya uchumi nchini Marekani hadi changamoto za siasa ya nje inayolikabili taifa hilo kutokana na vita nchini Iraq na Afghanistan.Alisema changamoto zinazowakabili ni nyingi na pamoja na kwamba haziwezi kutatuliwa kwa urahisi na katika kipindi cha muda mfupi lakini zitatuliwa.Aidha aliwakumbusha wamarekani kwamba umewadia wakati wao wa kusimama upya, kujifuta vumbi na kuanza tena kazi ya kuijenga Marekani.Rais Obama ambaye ana asili ya Kenya hakusita kuzikosoa sera za mtangulizi wake Goerge W Bush kuelekea vita dhidi ya Ugaidi na uchumi na kuuambia Ulimwengu kwamba sasa Marekani iko tayari kuongoza tena.

Kadhalika ameahidi kuimarisha uhusiano na ulimwengu wa kiislamu ambao umekuwa ukitia mashaka tangu kutokea mashambulio ya septemba 11 na pia kuwaonya viongozi wasiopenda amani wanaosababisha mizozo kwenye nchi zao na kuyabebesha lawama mataifa ya magharibi.

Aidha hotuba hiyo haikuyasahau mataifa maskini duniani Obama ametoa ahadi ya kuyanyooshea mkono wa msaada.Kwa upande mwingine ameonya viongozi wanaoendekeza rushwa kwamba hawana nafasi katika utawala wake.

Viongozi mbali mbali wa dunia wametoa pongezi zao kwa rais Obama Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Marekani kwa hali yoyote.

Barani Afrika pongezi nyingi kutoka kwa viongozi wa bara hilo,rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela amesema tukio hilo la kihistoria limemkumbusha furaha iliyotawala wakati alipoingia madarakani kama rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini humo mwaka 1994 baada ya kukaa jela miaka 27.

Katika barua yake aliyokabidhiwa Obama punde tu baada ya kuapishwa Mandela amemwabia rais huyo wa kwanza mwenye asili ya kiafrika nchini Marekani kwamba milele atabakia kuwa kipenzi katika nyoyo zao kwa kutimiza ndoto kubwa na kuleta sauti mpya ya matumaini.

►◄

 • Tarehe 21.01.2009
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GdGW
 • Tarehe 21.01.2009
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GdGW
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com