Shambulizi latokea Karibu na msikiti Madina | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Shambulizi latokea Karibu na msikiti Madina

Maafisa wanne wa polisi wameuawa nchini Saudi Arabia, baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kujiripua nje ya Msikiti wa Mtume mjini Madina shambulizi la tatu katika muda wa saa 24

Msikiti wa Mtume ulioshambuliwa ni wa pili kwa umuhimu katika dini ya kiislamu

Msikiti wa Mtume ulioshambuliwa ni wa pili kwa umuhimu katika dini ya kiislamu

Mshambuliaji huyo kwenye msikiti wa Mtume mjini Madina alijiripua baada ya polisi kuanza kumshuku na kumsogelea akiwa ndani ya gari lake, kwenye sehemu ya kuegesha magari mkabala na Msikiti wa Mtume, ambao ni wa pili katika sehemu takatifu sana kwenye ulimwengu wa kiislamu. Mbali na maafisa wanne waliouawa katika mripuko huo, wengine watano walijeruhiwa.

Huo ulikuwa mripuko wa tatu katika muda wa siku moja, takribani saa 24 tu kabla ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Awali, mshambuliaji mwingine aliulenga ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Jeddah ulio kwenye Bahari ya Sham, na mwingine aliulenga msikiti wa washia katika mji wa Qatif.

Tovuti ya habari ya Sabq ambayo iko karibu na Ufalme wa Saudi Arabia imesema mshambuliaji kwenye msikiti wa mtume huko Madina aliwalenga maafisa wa usalama wakati walipokuwa wakila futari.

Sala kama kawaida

Kituo cha televisheni cha al-Arabiya kinachomilikiwa na Saudi Arabia kimeripoti kuwa waumini walishiriki sala kama kawaida katika msikiti huo uliolengwa, na kilionyesha video ambazo kimesema ni za waumini hao, wakijazana katika ukumbi ulio mbele ya msikiti huo.

Maafisa wanne wa polisi waliuawa katika shambulizi la Madina

Maafisa wanne wa polisi waliuawa katika shambulizi la Madina

Kuna ripoti zinazokinzana kuhusu wahanga wa shambulizi kwenye msikiti wa washia wa Qatif, ambao mwezi Mei mwaka 2015 ulikumbwa na shambulizi jingine baya la kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS ambalo liliwauwa watu 22.

Tovuti ya Sabq imesema washambuliaji wawili walijiripua baada ya kushindwa kuufikia msikiti huo wa Faraj al-Omran, lakini msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Jenerali, Mansour al-Turki alisema alikuwepo mshambuliaji mmoja, na kuongeza kuwa maiti tatu zilikuwa eneo la mripuko.

Mashambulizi kwenye misikiti ya Madina na Qatif yalitokea kwa wakati mmoja, wakati watu walipokuwa wakijiandaa kufuturu.

Dola la kiislamu lashukiwa kuhusika

Ingawa bado hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo, kundi la IS ambalo Jumapili liliuwa watu 213 katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, limekuwa likilaani vikali serikali ya Saudi Arabia, inayoongozwa na familia ya kifalme.

Wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia imesema inashuku mashambulizi hayo yalifanywa na wapiganaji wa jihadi, na kulaani wale iliosema wamepotea njia, maneno ambayo aghalabu hutumiwa kumaanisha kundi la IS na mtandao wa al-Qaida.

Wizara ya mambo ya ndani ilimtambulisha shambuliaji aliyelenga ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah kama Abdullah Qalzar Khan, raia wa Pakistan aliyefanya kazi ya kuendesha gari, ambaye ameishi mjini Jeddah kwa muda wa miaka 12 pamoja na mkewe na wazazi wake.

Iran, ambayo ni hasimu wa Saudi Arabia katika Kanda ya Mashariki ya Kati imeyalaani mashambulizi hayo, ikisema magaidi wamekiuka miiko yote, na kutaka wasuni na washia waungane kuwapiga vita.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com