1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Shambulizi laua, kujeruhi Wapalestina wakisubiri msaada Gaza

Bruce Amani
29 Februari 2024

Shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel kwenye umati wa Wapalestina waliokuwa wakisubiri msaada wa kiutu katika Mji wa Gaza leo limewauwa na kuwajeruhi watu kadhaa.

https://p.dw.com/p/4d0pF
Mzozo wa Mashariki ya Kati| Rafah
Israel imetekeza maeneo makubwa ya Ukanda wa GazaPicha: Khaled Omar/Xinhua/picture alliance

Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa hospitali ya eneo hilo. Daktari Jadallah Shafai, mkuu wa idara ya wauguzi katika hospitali ya Shifa, ameiambia televisheni ya Al Jazeera kuwa karibu watu 50 wameuawa na 250 kujeruhiwa. Hakutoa idadi kamili ya vifo na majeruhi.

Televisheni hiyo imerusha video inayoonyesha miili kadhaa na watu waliojeruhiwa wakiwasili katika hospitali ya Shifa. Jeshi la Israel limesema linazichunguza ripoti hizo.

Soma pia: UN: Watu 576,000 wanakabiliwa na hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa ukanda wa Gaza

Hayo yanajiri wakati wapatanishi kutoka Misri, Qatar na Marekani wakipendekeza kusitishwa vita hivyo kwa muda wa wiki sita.

Wanatumai kwamba makubaliano hayo yanaweza kuanza mwanzoni mwa mwezi mtukufu kwa Waislamu wa Ramadhan ambao unatarajiwa kuanza Machi 10 au 11, kulingana na kuandama kwa mwezi kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu.