1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali yapanga mkakati wa miaka miwili ijayo

P.Martin24 Agosti 2007

Serikali ya muungano wa vyama vya Sozial Demokrat na Christian Demokrat iliyoshika madaraka miaka miwili iliyopita nchini Ujerumani,imefanikiwa kufanya mageuzi muhimu yaliyopangwa.

https://p.dw.com/p/CH9A
Kansela Merkel na baraza lake la mawaziri,nje ya Kasri la Meseberg
Kansela Merkel na baraza lake la mawaziri,nje ya Kasri la MesebergPicha: AP

Sasa,Kansela Angela Merkel amewakusanya mawaziri wake kwa mkutano wa siku mbili katika Kasri la Meseberg ukingoni mwa mji mkuu Berlin,kupanga miradi ya miaka miwili ijayo.

Baada ya kukutana kwa takriban saa 24 katika Kasri la Meseberg,Kansela Angela Merkel na mawaziri wake siku ya Alkhamisi,walitoa sura ya furaha na kuridhika.Viongozi hao wamekusanyika pamoja kujadili mipango ya kutekelezwa na serikali yao ya mseto katika miaka miwili ijayo.

Kansela Merkel anajikuta katika hali iliyoimarika kwani kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, bajeti ya serikali haina kasoro.Akifurahia hali hiyo Merkel alisema:

“Kwa muda mrefu hatukuwa na hali hii,lakini hatutaki tu kuridhika na mafanikio yaliyopatikana bali tunataka kupanga malengo ya miaka ijayo.“

Mradi mkuu wa Kansela Merkel unahusika na ulinzi wa mazingira.Miongoni mwa hatua zinazotazamiwa kutekelezwa ni kupunguza matumizi ya nishati katika kupasha joto nyumba,kupunguza idadi ya magari na vyombo vya majumbani vinavyotumia umeme ili kushusha kiwango cha gesi inayochafua mazingira.Azma ni kupunguza kwa asilimia 40 gesi ya kaboni dayoksaidi,ifikapo mwaka 2020, kulinganishwa na kile kipimo cha mwaka 1990. Waziri wa Mazingira wa Ujerumani,Sigmar Gabriel wa chama cha SPD na Waziri wa Uchumi,Michael Glos wa CSU,walifanikiwa kuondosha tofauti za maoni kati yao,muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo wa baraza la mawaziri siku ya Alkhamisi.

Na kuhusu suala la upungufu wa wataalamu katika soko la ajira,serikali imeamua kuondosha tatizo hilo.Katika siku zijazo kutakuwepo utaratibu utakaorahisisha kuwaajiri wanafunzi na wataalamu wa kigeni.

Hata hivyo lakini,bado kuna masuala ya mzozano kati ya wanachama wa Christian Demokrat na Social Demokrat.Kwa mfano,mada zinazohusika na malipo ya mshahara wa chini kabisa,bima ya ukosefu wa ajira na hata njia ya kupambana na upungufu wa wafanyakazi walio wataalamu katika sekta maalum. Hapo,kwa sehemu fulani,bado kuna tofauti za maoni kati ya pande hizo mbili.Lakini wanasiasa hao hawataki kupoteza wakati wa mkutano huo wa Meseberg kuyajadili masuala hayo kwa urefu.

Kwa maoni ya waziri wa ajira,Franz Münterfering,mkutano kama huu wa Meseberg unatoa nafasi ya kutazama kwa jumla,yale yanayopaswa kushughulikiwa kwa pamoja katika kipindi kijacho, ikiwa ni pamoja na sera za kisiasa.

Ni dhahiri kuwa miradi ya kisiasa inapaswa kushughulikiwa kwa upesi,kwani mageuzi yo yote yanahitaji kutekelezwa hadi mwezi wa Desemba. Kwani baadae ndio unaanza wakati wa kufanya matayarisho ya kampeni za uchaguzi.Mwakani kuna chaguzi muhimu za majimbo na katika mwaka 2009 vyama vya CDU na SPD vitapambana katika uchaguzi mkuu.