Serikali ya Zimbabwe yawaandama wapinzani | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Zimbabwe yawaandama wapinzani

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametoa wito wa umoja wakati akikabiliana na watu anaowatuhumu kuhujumu juhudi zake za kufufua uchumi wa nchi hiyo.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametoa wito wa umoja wakati akikabiliana na watu anaowatuhumu kuhujumu juhudi zake za kufufua uchumi wa nchi hiyo. Wachambuzi na wanaharakati wa upinzani wamepuuzilia mbali hotuba yake kuwa vitisho kwa raia. 

Katika hotuba hiyo isiyokuwa ya kawaida iliyochukuwa muda wa chini ya dakika 15 kupitia televisheni ya taifa, rais Emmerson Mnangagwa aliwalaumu mahasimu wake kwa matatizo yanayoikumba Zimbabwe na kusema hawataki kuiona serikali hiyo ikifanikiwa.

 Mnangagwa amesema kuwa  serikali yake imekumbwa na changamoto nyingi tangu ilipotawazwa na hii inajumuisha hali ya mgawanyiko kutoka kwa baadhi ya wapinzani, vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kinyume cha sheria, vimbunga, ukame na janga la virusi vya corona na kwamba itavishinda hila za kutatiza taifa hilo za baadhi ya mahasimu wanaoshirikiana na mataifa ya kigeni yasiotaka  maendeleo ya taifa hilo .

Hotuba hiyo inafuatia wiki zilizoshuhudia kukamatwa kwa wanaharakati wa kisiasa waliolengwa kwa madai ya kutoa wito wa maandamano dhidi ya umaskini na ufisadi. Tangu mwanzoni mwa wiki, hashtag #maishayaraiawaZimabwenimuhimu imekuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii kufuatia hatua ya kukamatwa kwa watu hao.

Maoni ya wanaharakati na wachambuzi kuhusiana na hotuba ya Mnangagwa

Makomborero Haruzivishe ni mmoja kati ya wanaharakati 14 wanaosakwa na polisi kwa kuitisha maandamano hayo ya Julai 31 dhidi ya serikali. Akizungumza kutoka eneo la siri, alipuuzilia mbali hotuba ya jana ya Mnangagwa na kusema haikuwa na maana ikilinganishwa na masuala yanayoikumba Zimbabwe kwa sasa. Haruzivishe ametaja masuala nyeti kuhusiana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, utekwaji nyara na kuzuiwa kwa uhuru wa raia. Ameongeza kuwa hawezi kusema katika demokrasia ya nchi hiyo kwa sababu hakuna demokrasia ya kuzungumzia.

Haruzivishe amesema kuwa hayo ndio masuala ya msingi ambayo yameenea katika kanda hiyo na kimataifa na kwamba  kutoka mbali nchini Jamaica, watu maarufu wanatuma ujumbe katika mtandao wa twitter kwamba maishayaraiawazimbabwenimuhimu lakini rais huyo hashughulikii masuala hayo na ndio watu wanataka kusikia.

Mwanaharakati huyo amesema kuwa rais huyo hakuonesha kujitolea kukabiliana na ufisadi hii ikiwa moja ya sababu ambazo watu wanasema mwanahabari Hopewell Chin'ono alikamatwa mwezi uliopita. Chin'ono na kiongozi wa upinzani Jacob Ngarivhume walikamatwa kwa madai ya kutoa wito wa ghasia mnamo Julai 31. Kwasasa wako gerezani wakisubiri uamuzi wa mahakama kuu siku ya Alhamisi wa kuwaachia huru kwa dhamana.

Mchambuzi mmoja huru Rejoice Ngwenya ametoa  maoni yake kuhusu hotuba ya Mnangagwa na kusema kuwa anawapa matumaini kwamba kuna jambo linaloendelea katika taifa.  Amesema rais huyo ameelezea kuhusu kile wanachokijuwa tayari na kwamba hali hiyo inaonesha hofu yake. Ngwenya amesema kuwa tukio hilo la Julai 31 limechochea wimbi la mageuzi katika serikali ya nchi hiyo na kwamba kuna jinamizi inayokabiliana nayo lakini haiko tayari kukubali.Baadhi ya raia wa Zimbambwe wanaohofia haki zao, waliandaika ujumbe katika mitandao yakijamii wakisema kuwa serikali huenda ikaimarisha mskao dhidi ya wapinzani.

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com