Serikali ya Yemen yashikilia zaidi ya wafungwa wa kisiasa 1,000 | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.10.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Yemen yashikilia zaidi ya wafungwa wa kisiasa 1,000

Repoti mpya ya Shirika la Haki za Binaadamu la Human Right Watch imemtaka Rais Ahmed Abdullah Saleh wa Yemen kuanzisha tume huru kuchunguza kukamatwa watu ovyo,kutoweka kwao na kuwawajibisha wanaohusika na vitendo hivyo.

Sehemu ya mji wa kale wa Yemen wa Sanaa ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo

Sehemu ya mji wa kale wa Yemen wa Sanaa ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo

Katika repoti hiyo ya kurasa 50 iliotolewa hivi karibuni shirika hilo la kutetea haki za binaadamu lenya makao yake nchini Marekani limechunguza zaidi ya kesi 62 za kutoweka kwa watu na kukamatwa kiholela kulikohusishwa na uasi wa Huthi kundi la kidini la madhehebu ya Shia nchini Yemen.

Kwa mujibu wa Hassan Zaid katibu mkuu wa chama cha upinzani cha Al Haq Al-Huthi Zaidi ambao wamechukuwa jina hilo kutoka kwa kiongozi wao Hussein Badraddin al Huthi wanakadiriwa kuwa kama asilimia 30 ya idadi ya watu wa Yemen.

Tawi jengine dogo la Zaidi ambalo ni kundi la Hashimi pia limekuwa likiandamwa kwa kukumatwa ovyo.

Uasi wa Huthi ulianza wakati wa uamsho wa vuguvugu la Wazaidi la kidini la madhehebu ya Washia kwa jina la Vijana Wanaoamini katika miaka ya 1990 chini ya uongozi wa al Huthi.Uasi wa Huthi dhidi ya serikali ulikuja kuripuka hapo mwaka 2004 kaskazini mwa Yemen ambapo serikali ilifunga shule za kidini.

Tokea kuanza kwa mzozo huo uliohusisha matumizi ya silaha kati ya serikali na waasi wa Huthi mashirika mbali mbali ya usalama nchini Yemen ikiwa pamoja na Usalama wa Kisiasa,Usalama wa Taifa na idara za kawaida za uchunguzi wa jinai zimekuwa zikiwashikilia mamia ya watu bila ya hati za kuwaruhusu kufanya hivyo na zimeshindwa kuwafungulia mashtaka yoyote yale ya jinai.

Mashirika ya haki za binaadamu ya Yemen yameorodhesha mamia ya kesi za watu kukamatwa ovyo kuhusiana na uasi huo.

Serikali inadaiwa kukamata watu wa familia wa Wahuthi wanaotafutwa ili kuwapa shinikizo wasalimu amri kwa serikali.Shirika la Haki za Binaadamu la Human Right Watch limepokea kesi tisa za aina hiyo.Wengine huwa wanafungwa kwa kuandika makala yenye kuelezea dhuluma za serikali wakati wa uasi huo.

Joe Stork naibu mkurugenzi wa shirika hilo kwa Mashariki ya Kati anasema madarzeni ya watu ambao hawakutenda uhalifu wowote ule bado wanaendelea kusota magerezani nchini Yemen miezi kadhaa baada ya rais wa nchi hiyo kuahidi kwamba atashughulikia kesi hiyo.

Amesema baadhi ya ndugu zao bado hawajuwi iwapo ndugu zao wapenzi waliotoweka wako hai au wamekufa.

Saleh ambaye amekuwa madarakani Yemen Kaskazini tokea mwaka 1978 na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Yemen tokea mwaka 1990 alitangaza kumalizika kwa mapigano katika jimbo la kaskazini la Sa'da hapo tarehe 17 mwezi wa Julai mwaka 2008.

Katika mwezi wa Augusti na Septemba Saleh aliamuru kuachiliwa kwa baadhi ya wafungwa lakini madarzeni wanaendelea kushikiliwa bila ya madai au kufunguliwa mashtaka na wengine hawajulikani walipo.Hapo mwezi wa Augusti mwaka 2008 serikali ilikiri kwamba inawashikilia zaidi ya wafungwa wa kisiasa 1,200.

Takriban katika kesi zote maafisa wanaokamata watu huwa hawajitambulishi au kumjulisha mtu wanayemkata au familia yake kwa nini anakamatwa na anapelekwa wapi.

Shirika ha haki za binaadamu la Human Right Watch linamtaka Rais Saleh wa Yemen atumie fursa hii kurekebisha dhuluma za vikosi vyake vya usalama na kuchukuwa hatua haraka kuhakikisha kwamba vitendo hivyo havirudiwi tena.

 • Tarehe 27.10.2008
 • Mwandishi Mohmed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FhTX
 • Tarehe 27.10.2008
 • Mwandishi Mohmed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FhTX
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com