Serikali ya Tanzania kuwachukulia hatua wanaomkashifu Rais Samia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Tanzania kuwachukulia hatua wanaomkashifu Rais Samia

Serikali ya Tanzania imesema itawachukulia hatua wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya uhalifu ikiwemo kumkashifu na kumtukana Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.

Kitendo hicho kinaelezwa na mamlaka za juu kuwa uvunjifu wa sheria na inaweza kusababisha machafuko ndani ya nchi wakati sheria zipo wazi kuhusiana na makosa hayo.

Kauli hiyo imetolewa siku ya Alhamisi na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, George Simbachawene wakati akizungumza katika mkutano na waandishi habari jijini Dodoma huku akisema kuwa tayari wamekwishawabaini watu walioko ndani na nje ya nchi ambao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya wizara ya mambo ya ndani kuchukua hatua kali za kisheria ili kuwashughulikia watu hao. 

Soma zaidi: Tanzania na kampeni dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao

Waziri Simbachawene ameongeza kusema, licha ya katiba ya Tanzania kutoa uhuru wa watu kujieleza na kutoa maoni yao lakini uhuru huo una mipaka yake na hivyo watu wanapaswa kuheshimu sheria za nchi na kwamba tayari watu hao wamekwishabainika ingawa Waziri huyo hakuwataja watu hao

Tansania George Simbachawene

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, George Simbachawene

Amesema kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ya 18 na 19 huku ibara ya 19 kifungu cha pili ikiweka masharti kwamba haki hiyo ya uhuru wa kutoa maoni itakuwa chini ya utaratibu kisheria kwa lengo la kutunza usalama, amani, maadili na Umoja wa kitaifa. Matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook, Instragram na Whatsapp yameelezwa na Waziri Simbachawene kuwa ndio inayotumika kufanya vitendo hivyo. 

Uhuru umevuka mipaka

Waziri huyo amesema kuwa uhuru huo unaotumika hivi sasa katika watu kujadiliana mambo mbalimbali umefikia hatua ambayo sasa ni tishio kwa uhuru wa watu wengine na maslahi ya taifa na kuongeza kuwa. 

Lakini wakati serikali ya Tanzania kupitia waziri huyo ikitoa taarifa ya kuwakamata wale wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya uhalifu katika mitandao ya kijamii , imeibua mjadala mkubwa kutoka kwa wachambuzi wa masuala ya haki za binadamu. Wachambuzi hao wanasema suala la kashfa lipo kwa asilimia kubwa sio rahisi kwenda mahakamani kusema kwamba kiongozi mkubwa amekashifiwa mtandaoni. 

Kwa muda sasa kumekuwepo na aina ya mijadala mbalimbali katika jamii kupitia kwenye mitandao ya kijamii, mijadala ambayo Waziri Simbachawene anasema ni kinyume na utaratibu uliowekwa na katiba wa uhuru wa mawazo.