1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria yaruhusu kuingizwa msaada wa kiutu

17 Februari 2016

Serikali ya Syria imetoa ruhusa ya misaada ya kibinadamu kupelekwa katika maeneo saba yaliyozingirwa, lakini matumaini ya kupatikana amani ya kudumu yamedidimia

https://p.dw.com/p/1HwbP
Syrien Hilfslieferungen Rotes Kreuz
Picha: Getty Images/AFP/A. Doumany

Hayo ni katika siku ambayo Uturuki imetowa wito wa kuanzishwa operesheni ya jeshi la nchi kavu katika nchi hiyo jirani iliyoharibiwa na vita

Misafara ya Umoja wa Mataifa inayopeleka misaada kwa maelfu ya Wasyria waliokwama katika miji iliyozingirwa imeanza leo, ikielekea katika miji kadhaa ukiwemo Madaya ambako watu kadhaa wanaaminika kufa kutokana na njaa.

Akizungumza mjini Damascus, mjumbe wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura amesema misafara ya msaada itatumwa leo katika kile kitakachokuwa ni mtihani wa ikiwa pande zinazozozana zitaruhusu kuingia misaada hiyo ya kiutu.

Syrien Damaskus UN Gesandter für Syrien Staffan De Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Takribani watu nusu milioni nchini Syria wako katika maeneo yaliyozingirwa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, baada ya karibu miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya serikali ya Syria na waasi.

Shirika la Hilali Nyekundu limesema misafara ya kwanza itaelekea katika vijiji vilivyozingirwa na waasi vya Fuaa na Kafraya katika upande wa Kaskazini, na Madaya na Zabadani, ambavyo vimezingirwa na jeshi.

Lakini mashambulizi ya makombora kwenye hospitali tano na shule mbili kaskazini mwa Syria ambayo Umoja wa Mataifa ulisema yaliwauwa watu 50 wakiwemo watoto, yamepunguza matumaini ya kutekelezwa mpango wa kusitisha mapigano uliofikiwa na mataifa yenye nguvu duniani mjini Munich wiki iliyopita. Chini ya makubaliano hayo, duru mpya ya mazungumzo itaandaliwa Geneva Februari 25.

Syrien Krieg Krankenhaus in Idlib
Mojawapo ya hospitali zilizoshambuliwa SyriaPicha: Syrian American Medical Society

Rais Barack Obama wa Marekani anasema itakuwa vigumu kuutekeleza mpango huo wa kuweka chini silaha ikiwa Urusi itaendeleza mashambulizi yake "Ukweli kwamba Putin hatimaye aliyapeleka majeshi yake na ndege zake na kuwekeza kabisa katika operesheni hii kubwa ya kijeshi sio ishara ya kuinyesha nguvu, bali kuonyesha udhaifu wa hali ya Assad. Kwamba ikiwa mtu ana nguvu, basi haupaswi kulituma jeshi lako kumsaidia mshirika wako".

Urusi ilikanusha kuwa iliishambulia hospitali yoyote, ikizitaja ripoti hizo kuwa ni “madai ambayo hayajathibitishwa”. Uturuki hata hivyo inasema mashambulizi ya angani ya Urusi ya kumuunga mkono Assad ni ya kinyama na sasa inashinikiza mpango wa kuwapeleka wanajeshi wan chi kavu nchini Syria kwa usaidizi wa Marekani na mataifa ya Ghuba.

Hapo jana, wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema Saudi Arabia imeanza tena mashambulizi ya angani ya muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria. Uturuki pia imejikita katika vita vyake na waasi wa Kikurdi kaskazini mwa Syria, ambao inaamini wana mafungamano na chama kilichopigwa mafuruku cha Wafanyakazi wa Kikurdi – PKK ambacho kimefanya uasi kwenye ardhi yake kwa miongo mingi. Urusi imesema mashambulizi hayo ya Uturuki ni ukiukaji mkubwa wa sheria.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba