Serikali ya Syria imefanikiwa kuokoa raia wake walioshikiliwa na magaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Syria imefanikiwa kuokoa raia wake walioshikiliwa na magaidi

Hatimaye serikali ya Syria imefanikiwa kuwahamisha wakazi elfu 5 wa mji wa Adra uliopo karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus, waliokuwa wamezingirwa na vikundi vya magaidi katika operesheni iliyofanywa na jeshi lake

Bendera ya Syria ikipepea katika mjini Damascus

Bendera ya Syria ikipepea mjini Damascus

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na jeshi la Syria, walipokuwa wakizungumza kupitia shirika la habari la serikali la Syria, SANA ni kwamba mpaka sasa wamefanikiwa kuokoa idadi kubwa ya wakaazi hao wa mji wa Adra waliokuwa wamezingirwa na magaidi waliokuwa na silaha, na sasa wapo katika mikono salama huku wakipatiwa huduma zote za kibinadamu na wizara ya ustawi wa jamii wa nchi hiyo.

Mpaka sasa haijafahamika vizuri ni namna gani raia hao walizingirwa na vikundi vya magaidi katika mji wao, uliopo upande wa kaskazini mashariki mwa mji wa Damascus, tarehe 11 mwezi huu.

Kwa mujibu wa mwangalizi wa shirika la haki za binadamu, ni kwamba inakadiriwa kumetokea vifo vya watu wapatao 32, wakati mapigano yalipoanza kati ya jeshi la serikali na magaidi hao waliochanganyika na wapiganaji wa kiislamu wenye itikadi kali.

Raia wengine wafa kwa njaa

Aidha Kwa mujibu wa ripoti iIiyotolewa na afisa wa shirika la misaada la Umoja wa Mataifa nchini Syria, Chris Gunness imefahamika pia kuwa licha ya watu waliokufa katika mashambulizi kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo na magaidi waliozingira mji wa Adra, watu wengine wapatao 15, wamefariki kutokana na kukosa chakula katika mji wa Yarmouk nchini Syria ,ambapo 10 kati yao walifariki katika eneo lililokuwa limeshikiliwa na magaidi.

Mwanamke wa kisyria aliyejeruhiwa na bomu wakati wa mapigano ya waasi na jeshi.katika mwa mji wa Allepo

Mwanamke wa kisyria aliyejeruhiwa na bomu wakati wa mapigano ya waasi na jeshi la nchi hiyo, katika mwa mji wa Allepo

Gunness amesema kuwa, kwashakoo ni miungoni mwa majanga yaliyowakumba wakazi wapatao elfu 2 wa mji wa Yarmouk nchini Syria, unaokaliwa na wakimbizi wengi kutoka Palestina, wakati nao walipokuwa wamezingirwa na vikundi vya magaidi tangu mwezi septemba na kufanya umoja wa mataifa kushindwa kupeleka misaada ya chakula.

Vikosi vya serikali vya Syria, vimezingira maeneo yote yanayotuhumiwa kukaliwa na magaidi, na kuwanyima raia wa maeneo hayo chakula,ili kuwashinikiza kuwafukuza magaidi miungoni mwao.

Lebanon kushambulia ndege za Syria

Wakati huohuo maafisa wa usalama wa Syria wamesema kuwa, vikosi vya Lebanon, vimezishambulia ndege za kivita za syria, zilizokiuka mamlaka ya anga ya Lebanon.hii ni mara ya kwanza kwa lebanon kufanya mashambulio hayo nchini syria, tangu nchi hiyo ilipoingia katika vita miaka kwa takribani miaka mitatu sasa.

Mwandishi: Diana Kago/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com