1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Sudan na kundi la waasi la JEM kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano

Kabogo Grace Patricia23 Februari 2010

Makubaliano hayo yanasainiwa huko Doha, Qatar na yatahudhuriwa na viongozi wa nchi kadhaa pamoja na maafisa wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/M9O7
Rais Omar al-Bashir wa Sudan.Picha: picture alliance / abaca

Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan na kiongozi wa kundi kubwa la waasi la Justice and Equality Movement-JEM, Khalil Ibrahim, jioni hii wanatarajia kutiliana saini makubaliano ya kusitisha mapigano. Makubaliano hayo yenye lengo la kumaliza mzozo katika jimbo la Darfur yatasainiwa kwenye mji mkuu wa Qatar, Doha.

Katika makubaliano hayo serikali ya Sudan imekubali kugawana madaraka na kundi la waasi la Justice and Equality Movement-JEM. Kipengele cha nne cha mkataba huo utakaosainiwa jioni hii huko Doha, unalitaka kundi la waasi la JEM kubadilisha mfumo wake na kuwa chama cha kisiasa mara tu baada ya kusainiwa makubaliano ya mwisho kati ya pande hizo mbili tarehe 15 Machi, mwaka huu kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Aprili. Rais Idriss Deby wa Chad na Mfalme wa Qatar, Sheikh Hammad bin Khalifa al-Thani, nchi ambazo zimekuwa zikifadhili mazungumzo ya amani kati ya Sudan na waasi wa Darfur, watahudhuria pia sherehe hizo za utiaji saini. Kabla ya sherehe za kutiliana saini makubaliano ya amani, Rais Deby na Mfalme Hammad watakuwa na mazungumzo pamoja na Rais Al-Bashir. Maafisa wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya watahudhuria pia sherehe hizo. Sehemu ya makubaliano hayo ya kusitisha mapigano ilisainiwa siku ya Jumamosi katika nchi jirani ya Chad. Mkuu wa Wakfu wa Kijerumani wa Friederich Herbert mjini Khartoum, Anja Dargatz, akizungumzia yanayotarajiwa kufikiwa huko Doha alisema, ''Inapaswa hapa kusisitizwa kwamba haya si makubaliano ya amani bali ni idhinisho na usimamishaji mapigano kama ilivyofikiwa nchini Chad siku ya Jumamosi.''

Hatua hiyo yapongezwa

Uingereza kwa upande wake imepongeza hatua ya pande hizo mbili kukubaliana kutia saini ya kusitisha mapigano na kugawana madaraka, huku ikizitaka pande zote kuongeza jitihada zao katika kupatikana kwa amani. Pongezi hizo zimetolewa leo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika, Bibi Glenys Kinnock, ambapo amesema kuwa Uingereza itaendelea kuunga mkono jitihada za kupatikana kwa usalama nchini Sudan. Wakati makubaliano hayo yanatarajiwa kusainiwa na kuridhiwa muda si mrefu ujao huko Doha, kundi la waasi la JEM leo limesema kuwa vikosi vya serikali vimewashambulia, ikiwa ni siku mbili baada ya sehemu ya makubaliano hayo kusainiwa huko Chad. Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na jeshi la Sudan.  Makundi mengine ya waasi likiwemo la Sudanese Liberation Army linaloongozwa na Abdelwahid Nur anayeishi uhamishoni, hadi sasa yamekataa kufanya mazungumzo na serikali ya Sudan.

Akizungumza jana usiku baada ya kuwasili mjini Doha, Rais Al-Bashir alisema kuwa mkataba huo utafungua njia ya kupatikana kwa amani na kumaliza vita vya Darfur vilivyodumu kwa miaka saba. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu 300,000 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 2.7 waliachwa bila makaazi. Hata hivyo serikali ya Sudan inasema ni watu 100,000 tu ndio waliuawa. Kutokana na mauaji hayo, mwezi Machi, mwaka uliopita, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ilitoa waranti wa kukamatwa Rais Al-Bashir kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita katika vita hivyo vya Darfur.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE/DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed