1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Libya yakanusha kuwa inasaidiwa na Uturuki

Zainab Aziz Mhariri: Yusra Buwayhid
29 Desemba 2019

Serikali ya Libya iliyopo mjini Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yakanusha kuwa inasaidiwa na kikosi cha waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki

https://p.dw.com/p/3VSj9
Türkei l Erdogan will Truppen nach Libyen schicken - Militär
Picha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ametahadharisha kwamba mgogoro wa nchini Libya unaweza kutumbukia katika vurumai na kwamba nchi hiyo inaweza kugeuka Syria nyingine. Waziri huyo Mevlut Cavusoglu amesema hayo wakati akifanya  juhudi kwa lengo la kupitisha sheria ya kuiwezesha Uturuki kupeleka majeshi nchini Libya.

Serikali ya Libya inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa imekuwa inakabiliana na majeshi ya jenerali muasi Khalifa Haftar yanayoungwa mkono na Urusi,Misri,Umoja  wa Falme za  Kiarabu na Jordan.

Waziri Cavusoglu amesema ikiwa Libya itageuka kuwa Syria nyingine na nchi zote za kanda  zitaathirika. Waziri huyo alisema hayo alipokuwa anahutubia kwenye mkutano wa chama  tawala nchini Uturuki AKP. Amesema inapasa kufanya kila linalopasa kuepusha vurumai na kugawaynika kwa Libya. Ameeleza kuwa hicho ndicho hasa kinachofanywa na nchi yake Uturuki. Ametamka kuwa Uturuki inashirikiana na serikali halali ya nchini Libya.

Majeshi ya jenerali muasi Haftar mpaka sasa bado hayajaweza kuingia mjini Tripoli lakini taarifa zinasema vikosi vyake vimepata mafanikio ya kiasi fulani kusini mwa mji huo kutokana na msaada wa wapiganaji kutoka Urusi na Sudan. Kwa mujibu wa taarifa za kidiplomasia ndege zisizokuwa na rubani za Umoja wa Falme za Kiarabu zimesaidia.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut CavusogluPicha: picture-alliance/dpa/TASS/A. Shcherbak

Ndege hizo zimemwezesha jenerali Haftar kudhibiti vita vya angani kwa sababu ndege hizo  zinadondosha mabomu mara nane zaidi kulinganisha na ndege zinazotumiwa na serikali halali ya Libya zinazotoka Uturuki. Mwezi uliopita Uturuki na serikali ya Libya GNA zilitiliana saini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya kijeshi na usalama na mkataba mwingine juu ya ulinzi wa miapaka ya baharini.

Wakati huo huo serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imekanusha madai  kwamba waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wanapigana bega kwa bega na  wanajeshi wa serikali hiyo. Tamko la kukanuhsa madai hayo limetolewa baada ya kinachodaiwa kuwa mkanda wa video uliowaonyesha waasi hao wakizungumza lahaja ya kiarabu cha Syria.

Siku ya Jumamosi shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria lilidai  kwamba waasi wa Syria wapatao 300 wanaoshiriiana na Uturukli waliwasili nchini Libya. Shirika  hilo limesema wapiganaji hao wamekusanyika kwenye kambi ya serikali ya Libya kwenye sehemu hatari ya kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Hata hivyo jeshi la Syria linalojiita la kitaifa linaloungwa mkono na Uturuki limekanusha madai hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Cavusoglu anatarajiwa kukutana na vingozi wa upinzani   siku ya Jumatatu na serikali ya Uturuki inatazamiwa kujadili mswaada juu ya kupeleka  majeshi  nchini Libya.

Wiki iliyopita Rais Erdogan alifahamisha juu ya uamuzi wa serikali yake kuhusu kupata ridhaa  ya bunge juu ya kupeleka majeshi ya Uturuki nchini Libya ili kuilinda serikali ya nchi hiyo  inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa ambayo inakabiliwa na kitisho cha vikosi vya jenerali  muasi Khalifa Haftar. Hatua hiyo imesababisha hofu, huenda mgogoro wa Libya ukatifua mgogoro wa kikanda.

Wakati huo huo Spika wa Bunge la Libya ameitaka jumuiya ya kimataifa ipinge uhalali wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambayo inashirikiana na Uturuki.

Vyanzo: (RTRE/DPA)