Serikali ya Afghanistan yapandisha mishahara katika kukabiliana na rushwa | Masuala ya Jamii | DW | 18.11.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Serikali ya Afghanistan yapandisha mishahara katika kukabiliana na rushwa

Serikali ya Afghanistan ambayo bado inakabiliana na vita kutokana na kuendelea uasi wa kitalibani, imeanzisha vita vingine dhidi ya rushwa. Katika juhudi za kukomesha tabia hiyo mbaya, serikali ya rais Hamid Karzai, ilichukuwa hatua ya kupandisha mishahara ya wafanyakazi wake.

Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai

Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai

Kulingana na hatua hiyo, mshahara wa kiwango cha chini kabisa kwa mfanyakazi wa serikali utakuwa wa dolla 80 kwa mwezi huku mshahara wa kiwango cha juu kabisa utakaopewa maafisa wakuu wa serikali ni dolla 800.

Wafanyakazi wa serikali nchini Afghanistan wanapokea mshahara kidogo kulinganisha na kiwango cha mshahara wa kiasi ya dolla 2,000 unaotolewa na mashirika kadhaa yasioegemea serikali ama NGO’s kwa wafanyakazi wao na watu wa kujitolea wanaoshirikiana na mashirika hayo.

Hata wafanyakazi wa kiufundi wanapokea mara tatu zaidi ya mshahara mfanyakazi wa ofisini.

Hali hiyo ilitajwa kuwa sababu muhimu ya kutapakaa rushwa na wafanyakazi wengi kushindwa kuajibika.

Katika mahojiano na gazeti la Fortune magazine, rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, alikiri na hapa ninamnukuu

´´Rushwa umeenea katika mfumo mzima wa nchi´´.

Mwisho wa kumunukuu rais Karzai.

Sasa kuna matumaini kwamba mpango huo mpya wa malipo utaboresha hali ya kimaisha ya wafanyakazi na kuongeza motisha kazini katika taasisi za serikali.

Rushwa ni changa moto kubwa inayoikabili serikali ya Afghanistan. Rais Hamid Karzai alitangaza rasmi vita dhidi ya rushwa kwa kiwango fulani kufuatia lawama zinazozidi kupanda kutoka kwa vyombo vya habari vya kitaifa na vya kigeni pamoja na nchi fadhili. Tume ziliundwa katika ofisi na taasisi za serikali kupambana na rushwa.

Lakini kile ambacho kingesaidia zaidi, ni kuwachunguza kwa makini na kuwaondoa wale wanaokula rushwa pamoja na kuweka utaratibu wa kisheria, linasema gazeti huru la ´´Killid Weekly ´´ katika uhariri wake.

Gazeti hilo linaendelea kusema: Operesheni ya kuwaondoa walaji mlungula unafaa kuanzia katika ngazi ya juu kwa wanasiasa na maofisa wa serikali. Kuwafuatilia na kuwafukuza wafanyakazi wa kawaida hakutasaidia kulisuluhisha tatizo hilo.

Isitoshe, nyadhifa na viwango vya mishahara vyapaswa kutolewa kwa msingi wa kuajibika kwa mfanyakazi na wala sio kwa upendeleo.

Magazeti nchini Afghanistan yanasema kuwa mwanasheria mkuu nchini humo, Jaber Sabat hivi karibuni alianzisha kampeni ya kupambana na rushwa lakini juhudi zake zinakwamishwa na viongozi wa ngazi ya juu.

Maofisa wakuu wa serikali wanaohusika na kashfa za rushwa hukingiwa kibawa kama vile kiongozi wa polisi wa uhamiaji kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Kabul, Amin Amarkheil ambae alihusika katika mkasa wa biashara haramu ya madawa ya kulevya.

Kuenea kwa rushwa kulilichafua jina la Afghanistan, kukashusha umarufu wa serikali miongoni mwa raia na kuzusha lawama kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Benki ya dunia iliiruhusu serikali ya Afghanistan ipandishe mishahara ya wafanyakazi wake. Mnamo mwezi Oktoba, uongozi wa majeshi ya jumuiya ya NATO ya kuweka amani nchini Afghanistan, ulionya kuwa ikiwa maisha ya raia wa kawaida hayataboreshwa kwa muda wa miezi 6 ijayo, kutakuwa na watu wengi ambao watakuwa tayari kujiunga na waasi wa kitalibani.

Pamoja na kuruhusu kupandishwa mishahara ya wafanyakazi, Benki ya dunia iliisihi serikali ya Afghanistan kuanzisha ukarabati katika maeneo ya kusini mwa nchi ambako waasi wa kitalibani wanaendelea na harakati zao.

 • Tarehe 18.11.2006
 • Mwandishi Gregoire Nijimbere
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHm7
 • Tarehe 18.11.2006
 • Mwandishi Gregoire Nijimbere
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHm7
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com