Serikali mpya ya Marekani itafanikiwa kuleta amani ya haki Mashariki ya Kati? | Magazetini | DW | 06.01.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Serikali mpya ya Marekani itafanikiwa kuleta amani ya haki Mashariki ya Kati?

Mapigano katika Ukanda wa Gaza ni mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani sawa na mpango wa pili wa serikali kusaidia kupiga jeki uchumi uliodorora.

Tukianzia Mashariki ya Kati gazeti la MANNHEIMER MORGEN linasema:

Israel wala haina azma ya kuvimaliza haraka vita vinavyopiganwa kwenye Ukanda wa Gaza.Mashambulizi ya vikosi vya nchi kavu yalianzishwa siku ya Jumamosi na mapigano hayo yatasitishwa pale lengo la vita hivyo litakapotimizwa - yaani kulizima kundi la Hamas.Na wanamgambo wa Hamas ndio wanaendelea kujikinga na kurusha maroketi dhidi ya Israel. Wanamgambo hao wapo tayari kupigana mpaka risasi ya mwisho itakapomalizika.Kwa hivyo operesheni ya majeshi ya Israel itakuwa ndefu.

Gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

Wajumbe watatu,wakati mmoja,wapo mbioni huko Mashariki ya Kati.Waziri wa Mambo ya Nje Schwarzenberg wa Jamhuri ya Czech iliyoshika urais wa Umoja wa Ulaya mwezi huu;Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na mjumbe maalum kwa Mashariki ya Kati Tony Blair.Kwa maoni ya Nürnberger Zeitung ujumbe huo hautazamiwi kufua dafu - matumaini yote yapo kwa viongozi wapya watakaoshika madaraka nchini Marekani kuwa juhudi zao zitaleta amani ya haki katika Mashariki ya Kati.

Tukigeukia mpango wa pili wa msaada wa serikali ya Ujerumani kufufua uchumi uliozorota gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linaamini kuwa wafanyakazi walipaswa kupunguziwa kodi ya mapato tangu muda mrefu.Linaongezea:

Tangu miaka na miaka,waajiriwa kila walipoongezewa mishahara,walijikuta wakilipa kodi zaidi bila ya serikali kuchukua hatua ya kuwapa nafuu ya kifedha kwa njia nyingine.Gazeti hilo linapinga dai la chama cha Social Democrat kuwa wanaopokea mishahara mikubwa ndio watakaonufaika na mpango huo mpya wa serikali.Kwa maoni ya Sächsische Zeitung, watakaonufaika kwanza kabisa ni wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya chini na ya wastani-yaani wale walio uti wa uchumi wa Ujerumani.Na hao ndio wanaofanyakazi kwa bidii na kuchangia kujenga uchumi wa Ujerumani.

Gazeti la NORDSEE ZEITUNG vile vile linakaribisha hatua ya kuwapunguzia wananchi kodi ya mapato.Wakati huo huo lakini linakumbusha:

Kupunguziwa kodi kwa baadhi ya wafanyakazi humaanisha kuwa nafuu watakayopata kwa mwaka,haitofikia hata Euro 100.Hiyo wala haitosaidia kuhamasisha watu kununua zaidi wala kufufua uchumi lamalizia gazeti la NORDSEE ZEITUNG kutoka Bremerhaven.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com