Serikali mpya Libya kuidhinishwa | Matukio ya Afrika | DW | 15.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Serikali mpya Libya kuidhinishwa

Bunge linaloyajumuisha makundi hasimu lilitangaza kuundwa kwa baraza la mawaziri, baada ya serikali ya awali kukataliwa mwezi Januari na sasa inatazamiwa kuwa itapitishwa rasmi.

Bunge la Libya kwa ajili ya serikali isiyotambuliwa kimataifa ya mjini Tripoli.

Bunge la Libya kwa ajili ya serikali isiyotambuliwa kimataifa ya mjini Tripoli.

Miaka kadhaa ya mzozo wa kisiasa na kivita tangu kuangushwa madarakani na kuuawa kwa Rais Muammar Gaddafi mwaka 2011 imeigawa nchi hiyo kati ya serikali hasimu na kusambaza ghasia zinazoongozwa na wanamgambo wenye silaha waowania madaraka.

Taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kaskazini mwa Afrika na linalologawana mpaka wa Bahari ya Mediterrenia na Ulaya limegeuka sasa kuwa kimbilio la kundi la kigaidi lijiitalo "Dola la Kiislamu".

Wajumbe wa bunge linalotambuliwa kimataifa lenye makao yake kwenye mji wa mashariki wa Tobruk, walisema wanatarajia kura kupigwa jioni ya Jumatatu. "Wabunge wako njiani kuelekea bungeni na matayarisho yanaendelea. Upigaji kura utafanyika leo," mbunge Ali Takbali aliliambia shirika la habari la AFP.

Kuidhinishwa kwa baraza hilo la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu mteule Fayez al-Sarraj, itakuwa hatua muhimu sana katika kuukwamua mkwamo wa kisiasa na kuhitimisha miezi kadhaa ya jitihada kubwa na ngumu sana za kidiplomasia.

Umoja wa Mataifa wataka serikali iundwe

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Martin Kobler, aliwatolea wito wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunga mkono serikali hiyo mpya.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Martin Kobler.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Martin Kobler.

"Safari ya kuelekea amani na umoja wa watu wa Libya hatimaye imeanza," aliandika Kobler kwenye mtandao wa Twitter.

"Ni jambo muhimu sana kwamba sasa Baraza la Wawakilishi linaiidhinisha serikali hii ya umoja wa kitaifa. Ni fursa pekee ya amani ambayo haistahiki kuipoteza."

Kile kinachoitwa Baraza la Urais lililopewa jukumu la kuunda serikali mpya, liliipitia upya orodha mpya baada ya bunge kulikataa baraza lenye mawaziri 32, likisema ni wengi sana. Baraza hilo lilitoa siku 10 kuwa muda wa mwisho wa kuwasilishwa kwa baraza jipya la mawaziri ambao ulimalizika Jumapili.

"Tunatazamia kwamba hatua hii itakuwa mwanzo wa mwisho wa vita nchini Libya," mjumbe wa baraza hilo, Fathi al-Marjebi, alisema siku ya Jumapili akiwa mjini Skhirat, Morocco, ambalo baraza hilo limekuwa lilikikutana.

Orodha mpya itakuwa na mawaziri 18 na Mahdi al-Barghati atakuwa waziri wa ulinzi, nafasi ambayo ilikuwa kikwazo kikubwa kwenye mazungumzo. Licha ya Barghati kuwa mtu wa karibu na serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa, uteuzi wake ulikuwa ukipingwa na mkuu wa jeshi mwenye nguvu sana, Jenerali Khalifa Haftar.

Hata hivyo, hata kwenye Baraza lenyewe la Urais bado kuna mgawanyiko hadi sasa. Wajumbe wawili kati ya tisa wa baraza la urais walikataa kuiidhinisha serikali hiyo, ingawa wabunge waliliambia shirika la habari la AFP kwamba wapinzani wa mpango huo ni wachache.

Thuluthi mbili ya wabunge wanahitajika kuyaridhia makubaliano jumla ya kisiasa na kisha wingi mdogo kupitisha kura ya imani kwa serikali hiyo mpya.

Serikali inayotambuliwa kimataifa ina makao yake makuu mashariki ya Libya baada ya kuukimbia mji mkuu Tripoli ambao ulichukuliwa na muungano wa makundi ya wanamgambo mwezi Agosti 2014. Muungano huo una serikali yake yenyewe na bunge unaoliita "Baraza Kuu la Taifa", ambapo robo nzima ya wajumbe wake waliunga mkono makubaliano ya serikali ya pamoja yalipofikiwa mwezi Disemba, lakini idhini yake rasmi haihitajiki kwa serikali hiyo kuweza kuanza kazi.

Kitisho cha kuimarika "Dola la Kiislamu"

Makubaliano hayo ya kugawana madaraka yamekuwa yakipewa umuhimu mkubwa kutokana na hofu kwamba huenda kundi la kigaidi la "Dola la Kiislamu" linajiimarisha nchini Libya, baada ya kubanwa vikali nchini Syria na Iraq.

Moja ya matangi ya mafuta yakiripuka moto katika bandaji ya al-Sidra.

Moja ya matangi ya mafuta yakiripuka moto katika bandaji ya al-Sidra.

Kundi hilo la itikadi kali limechukuwa udhibiti wa mji wa Sirte alikozaliwa Gaddafi na kufanya mashambulizi makali dhidi ya mahasimu wao, yakiwemo mashambulizi ya kujitoa muhanga, ambayo yameuwa watu kadhaa katika miezi ya hivi karibuni.

Pia limepiga hatua kubwa kwenye kutwaa baadhi ya vituo vya mafuta nchini Libya, taifa ambalo linakisiwa kuwa na akiba ya matangi bilioni 48 ya mafuta, akiba kubwa kabisa barani Afrika.

Wanadiplomasia wa kimataifa wamekuwa wakiongeza shinikizo lao kwa maafisa wa Libya kukamilisha uundaji wa serikali ya pamoja na huku wakielezea wasiwasi wao kutokana na kuimarika kwa ushawishi wa "Dola la Kiislamu."

Kwenye mkutano wao wa Rome wa mwezi Februari, wanadiplomasia wa ngazi za juu kutoa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq walikataa wito wa kuingia kijeshi nchini Libya, wakisisitiza haja ya utulivu wa kisiasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com