Seleka yadai kugawiwa kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati | Matukio ya Afrika | DW | 23.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Seleka yadai kugawiwa kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Waasi wa Seleka wamedai Jamhuri ya Afrika ya Kati igawiwe pande mbili kaskazini kwa Waislamu na kusini kwa Wakristo madai ambayo ni ya kushangaza waliyoyatowa katika mazungumzo ya kukomesha ghasia za kidini nchini humo.

Wapiganaji wa Seleka Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wapiganaji wa Seleka Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mkuu wa ujumbe wa Seleka katika mkutano huo wa siku tatu mjini Brazavvile Generali Mohamed Moussa Dhaffane ameuambia mkutano huo kwamba wakati umefika wa kuigawa rasmi nchi hiyo baada ya maelfu ya Waislamu kukimbia kutoka kusini mwa nchi hiyo.

Mazungumzo hayo ya Brazzavile yanayowakutanisha wajumbe 169 kuanzia wa serikali ya mpito,mashirika ya kiraia na makundi ya wapiganaji yana lengo la kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kusalimisha silaha za waasi wa Seleka ambao wengi wao ni Waislamu na wanamgambo wa Kikristo wa anti-balaka.

Maelfu wameuwawa na zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na machafuko hayo ya kidini ambayo yalizuka nchini humo baada ya wapiganaji wa Seleka kunyakuwa madaraka hapo mwezi wa Machi mwaka 2013 katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi.

Utawala wa Seleka

Aliekuwa kiongozi wa Seleka na rais wa mpito Jamhuri ya Afrika ya Kati Michel Djotodia.

Aliekuwa kiongozi wa Seleka na rais wa mpito Jamhuri ya Afrika ya Kati Michel Djotodia.

Baada ya utawala wa Seleka wa miezi 10 uliokumbwa na uporaji mateso na mauaji kiongozi wa Seleka na aliyekuwa rais wa mpito Michel Djotodia alijiuzulu chini ya shinikizo la kimataifa.

Wanamgambo wa Kikristo walizidisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Waislamu na kuwatimua waasi pamoja na raia wa Kiislamu hadi kaskazni mwa nchi hiyo na kuleta hali ya kugawika kwa taifa hilo iliopo hivi sasa.

Abakar Sabone waziri wa zamani ambaye ni Muislamu na kiongozi wa vuguvugu la MLCJ ambaye alikuwako katika mkutano wa Brazzaville amesema Seleka wameweka sharti la kuendelea na mazungumzo hayo kwa kutaka nchi hiyo igawiwe pande mbili.

Sabone amesema Seleka wanaiwakilisha jamii ya Waislamu walioko kaskazini mwa nchi hiyo na kwamba nchi hiyo tayari imegawika kwa sababu Waislamu wote hivi sasa wako kaskazini na serikali iliopo sasa haina uwezo wa kufikia kaskazini. Ameongeza kusema Seleka wanakieleza kile inachokitaka jamii ya kaskazini.

Dai la kuigawa nchi laleta mshtuko

Mojawapo ya maandamano ya kudai usalimishaji wa silaha Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mojawapo ya maandamano ya kudai usalimishaji wa silaha Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wito wa kuigawa nchi hiyo umekuja kuwashangaza wajumbe wa upatanishi katika mkutano huo akiwemo Rais wa Jamhuri ya Congo Denis Sassou N'Guesso ambaye ndio mwenyekiti wa mkutano huo.Inaelezwa kwamba N'Guesso alirusha kalamu yake mezani kwa ghadhabu baada ya kutolewa kwa dai hilo la kuigawa nchi hiyo.

Maafisa wa Seleka,serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na wapatanishi hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo ya Seleka.

Jean Marie Michel Makoko mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ameliambia shirika la habari la Uingereza kwamba kwa sasa suala hilo la kuigawa nchi hiyo halimo katika mjadala.

Ameongeza kusema kwamba suala hilo litaweza kujadiliwa huko mbele iwapo fikra hiyo ya kuigawa litakuwa takwa la dhati na kwamba kwa vyoyote vile kwa sasa hawana utashi nalo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters

Mhariri : Josephat Charo