1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz asema Ukraine itahakikishiwa usalama

Mohammed Khelef
2 Machi 2023

Ujerumani imesema inajumuika na washirika wake kwenye mazungumzo na Ukraine juu ya hakikisho la kiusalama kama sehemu ya matayarisho ya amani endelevu kwa taifa hilo lililovamiwa na Urusi kwa mwaka mzima sasa.

https://p.dw.com/p/4O9Ue
Deutschland | Bundestag Bundeskanzler Scholz Regierungserklärung Zeitenwende
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akizungumza kwenye bunge la shirikisho, Bundestag, mjini Berlin siku ya Alkhamis (Februari 2), Kansela Scholz alisema kwamba ni wazi kuwa raia wa Ukraine na serikali yao wanataka amani ya nchi yao na ni jukumu la dunia kuwahakikishia watu wa Ukraine usalama wao.

"Raia wa Ukraine walitaka vita hivi vimalizike tangu siku ya kwanza vilipoanza. Kila raia wa nchi hiyo anataka amani zaidi kuliko mtu mwengine yeyote. Lakini njia kuelekea amani hiyo imejidhihirisha kuwa ngumu kuiandama. Kupata amani kunamaanisha pia kupambana na uchokozi huu na kukabiliana na dhuluma inayotendwa dhidi yao," alieleza kiongozi huyo.

Soma zaidiZelensky ashinikiza uharakishaji wa kuepeleka silaha Ukraine

Kutokana na hilo, Scholz alisema Ujerumani ilikuwa inazungumza na Kyiv pamoja na washirika wengine juu ya hakikisho la kiulinzi kwa Ukraine, ingawa alisisitiza kuwa hakikisho hilo litawezekana tu ikiwa Ukraine itafanikiwa kujilinda kwenye vita vinavyoendelea. 

Kansela huyo wa taifa kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya aliwaambia wabunge kwamba serikali yake ingeliendelea kuisaidia Ukraine kwa kuipa silaha, kwa kuwa Rais Vladimir Putin ameonesha wazi kwamba dhamira yake ya kujitanuwa haitamalizikia Ukraine pekee.

"Putin ameonesha kwa hatua yake hii anataka kubadili ramani ya mataifa. Lengo lake ni kuitikisa misingi ya Ulaya. Anataka kuifuta mipaka ya Ukraine na kuliharibu kama taifa. Hilo halitawachwa litokee." Alisema Scholz.

Kidole kwa China

Deutschland Berlin | Bundestag | Regierungserklärung Olaf Scholz, Bundeskanzler
Kansela Olaf Scholz akihutubia kwenye bunge la shirikisho, Bundestag, siku ya Alkhamis ya tarehe 2 Machi 2023.Picha: Christian Spicker/IMAGO

Hotuba hii ya Kansela Scholz iliyodhamiriwa kuelezea sera mpya ya nje ya Ujerumani kuelekea ulinzi na usalama, ilikuja ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine, na wakati Berlin ikiwa imeongeza kiwango ya uwekezaji wake kwenye jeshi lake, imepunguza mafungamano ya kiuchumi na Urusi na kuvunja msimamo wake wa muda mrefu wa kutokutuma silaha kwenye maeneo yenye vita. 

Badala yake, Scholz aliionya China, taifa la pili kwa nguvu za kiuchumi na kijeshi duniani, kwamba isiingie kwenye mtego wa vita wa Urusi kwa kulisaidia taifa hilo kwa silaha, bali isaidie kuleta amani.

Soma zaidiZelensky: Urusi yaendeleza mashambulizi mashariki ya Ukraine

"Ujumbe wangu kwa Peking uko wazi: Tumieni ushawishi wenu kwa Moscow kushinikiza kuondoka kwa vikosi vya Urusi, na musipeleke silaha kwa mvamizi." Alisema.

Wachambuzi wanasema kauli hii ya Scholz inaweka bayana mpasuko mkubwa uliopo miongoni mwa mataifa makubwa duniani, ambapo China na India zimeendelea kukwepa kulaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, huku mataifa ya Magharibi yakishirikiana kwa hatua za kisiasa, kiuchumi na kijeshi.

Vyanzo: Reuters, dpa