1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yapiga marufuku huduma ya Blackberry.

6 Agosti 2010

Kuna wateja milioni 46 wanaotumia huduma ya simu aina ya Blackberry kote duniani.

https://p.dw.com/p/OdYB
Wateja laki saba walikuwa wakitumia huduma ya Blackberry nchini Saudi Arabia.Picha: dpa

Saudi Arabia imesimamisha huduma ya aina ya simu ya Blackberry, huku hali ya wasiwasi ikitanda katika kanda ya mashariki ya kati na maeneo mengine barani Asia kuhusu usalama wa huduma hiyo.

Mataifa mengine kama India, Lebanon na Algeria yanazingatia kulidurusu suala hilo zito la mawasiliano na hofu kwamba ni kitisho cha usalama.

Saudi Arabia ilitoa amri wiki hii kwamba tume ya mawasiliano na teknolojia katika ufalme huo ikomeshe huduma hiyo ya simu aina ya Blackberry na kwamba makampuni yanayotoa huduma hiyo yasipofuata amri hiyo yatatozwa faini ya Dola milioni 1.3.

Taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la SPA nchini humo ilisema kwamba kulingana na jinsi huduma hiyo inavyotolewa hivi sasa, haiambatani na utaratibu wa udhibiti wa tume hiyo na masharti yanayofaa kufuatwa ya kutoa leseni ya kazi.

Mfumo wa siri wa huduma ya kutuma na kupokea barua pepe unahifadhiwa katika mitambo maalum ya kuhifadhi habari nchini Canada ambayo ni makao makuu ya kampuni inayotoa huduma hiyo, na kwamba watu wengine, yakiwemo mawakala wa ujasusi, hayawezi kufuatilia mawasiliano na hata wahalifu na waasi wanaweza kupata mawasiliano hayo.

Kuna zaidi ya wateja laki saba wanaotumia huduma hiyo nchini Saudi Arabia, ufalme ambao unafuatilia sana suala la usalama, maadili ya Kiislamu na unadhibiti matumizi ya huduma ya mtandao wa Internet.

Kusimamishwa huko kwa huduma hiyo kunajiri baada ya ufalme huo wa Kiarabu kusema kwamba utasitisha huduma ya simu hiyo ya Blackberry katika taifa hilo la ghuba kuanzia tarehe 11 mwezi Oktoba kutokana na wasiwasi wa usalama.

Lebanon, India na Kuwait pia zimejitokeza na kuelezea wasiwasi kuhusu usalama wa matumizi ya huduma hiyo ya Blackberry ambayo ina wateja milioni 46 kote duniani.

Mwelekeo huo sasa umeifanya Marekani kuingilia kati, na waziri wa mambo ya kigeni, Hillary Clinton, alisema atafanya mazungumzo na mataifa ya Kiarabu kutafuta suluhisho linalofaa.

Alisema wanachukua muda kushauriana na kutathmini vipengee vyote vinavyojitokeza kwa sababu wanajua ukweli kwamba kuna kitisho cha usalama. Hadi kufikia sasa, kampuni inayotoa huduma hiyo ya simu aina ya Blackberry, iitwayo RIM ,yaani Research in Motion, haijatoa taarifa kuhusu pigo hilo la kibiashara.

Mwandishi, Peter Moss /AFP/Reuters

Mhariri, Othman Miraji