1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yaanza kuwasafirisha wafungwa wa Kihouthi

Sylvia Mwehozi
6 Mei 2022

Muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia umeanza kuwasafirisha wafungwa walioachiwa kuelekea Yemen kwa kushirikiana na kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC.

https://p.dw.com/p/4AwWj
Gefangenenaustausch im Jemen
Picha: Hani Mohammed/AP Photo/picture-alliance

Muungano huo ulisema mwezi uliopita kwamba utawaachia wafungwa 163 wa kundi la Kihuthi linaloungwa mkono na Iran ambao wamekuwa wakipambana na Saudi Arabia. Lakini, mapema mwezi huu mkuu wa kamati ya masuala ya gereza wa kundi la Kihouthi, alisema orodha hiyo ina majina ya watu wasiowafahamu na ambao si miongoni mwa wafungwa wao.

Msemaji wa Kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC nchini Yemen Bashir Omar, amelieleza shirika la habari la Reuters kwamba wafungwa 108 walioachiwa watasafirishwa kutokea Saudi Arabia kuelekea mji wa kusini wa bandari wa Aden, ambako serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudia ina makao yake makuu na 9 watapelekwa mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na Wahouthi.

Jemen Huthi-Rebellen in Sanaa
Wapiganaji wa Kihutuhi wa YemenPicha: imago/Xinhua

Taarifa ya Muungano huo wa kijeshi inasema ndege mbili tayari zimeondoka kuelekea Yemen huku ya tatu ikitarajiwa nayo kuanza safari. Wapiganaji wa kigeni watakabidhiwa kwenye balozi zao, limeripoti shirika la habari la Saudia SPA, bila ya kutoa maelezo utaifa wa wapiganaji hao wa kigeni au idadi yao.

Afisa mmoja katika serikali ya Yemen naye alipozungumza na shirika la Reuters amedai kwamba Wahouthi walikubali kuwapokea wafungwa 9 pekee kwahivyo waliobakia wanasafirishwa hadi Aden.

Iran yasema mashambulizi ya Houthi dhidi ya Saudia ni onyo

Muungano wa kijeshi uliingilia kati vita vya Yemen mnamo mwaka 2015dhidi ya Wahouthi baada ya kundi hilo kuiondoa madarakani serikali inayotambulika kimataifa mjini Sanaa mwishoni mwa mwaka 2014. Pande zinazozozana zilifikia makubaliano ya miezi miwili yaliyoanza kufanya kazi Aprili 2, ikiwa ni mafanikio ya kwanza makubwa katika vita vya miaka mingi. Makubaliano hayo yalifikiwa chini ya juhudi za Umoja wa Mataifa za kukomesha vita ambavyo vimewaua maelfu ya watu na kusababisha mgogoro mbaya wa kibinaadamu.

Mamlaka kutoka pande hizo mbili zimekuwa zikiripoti juu ya ukiukwaji wa karibu kila siku wa makubaliano ya usitishaji mapigano, hususan katika mji mkuu wa iliko serikali wa Marib ambao Wahouthi wamejaribu kuudhibiti kwa zaidi ya mwaka.

Pande hizo pia zilikuwa zimejadiliana juu ya uwezekano wa kubadilishana wafungwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa ambao ungewahusisha wafungwa 1,400 wa Kihouthi na wafungwa 823 wa Muungano huo wa kijeshi wakiwemo raia 16 wa Saudia. Mabadilishano mengine kama hayo yalifanyika mwaka 2020 na kuwahusisha wafungwa takribani 1,000.