1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia: Wauaji wa Khashoggi kuhukumiwa kifo

Amina Mjahid
15 Novemba 2018

Wakati Saudi Arabia ikitaka hukumu ya kifo kutolewa kwa watu watano wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi Uturuki imesema hatua zilizotangazwa ni nzuri lakini hazitoshi.

https://p.dw.com/p/38K15
Proteste in den USA nach Mord an Jamal Khashoggi
Picha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Jamal Khashoggi, mwanahabari wa gazeti la Marekani la Washington Post na mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin Salman aliuwawa na mwili wake kukatwakatwa, na kisha kukabidhiwa afisa mmoja nje ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia ulioko mjini Istanbul,  alisema msemaji wa mwendesha mashtaka mkuu katika tamko la kwanza la Saudi Arabia kukiri namna mwanahabari huyo alivyouwawa.

Portraitfoto: Mohammed bin Salman
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Picha: picture-alliance/AP/A. Nabil

Lakini msemaji huyo Shaalan al-Shaalan amekanusha kwamba mwanamfalme Mohammed bin Salman alifahamu juu ya mauaji hayo.

Mwendesha mashtaka amependekeza hukumu ya kifo kwa washukiwa wote watano, waliofunguliwa mashtaka ya kuamuru na kutekeleza uhalifu huo na hukumu nyengine kali kwa watu wengine watakaohusika na mauaji ya mwanahabari huyo. 

Mwendesha mashtaka amesema tayari watu 21 wamekamatwa huku wengine 11 wakisadia katika uchunguzi unaoendelea. Awali Saudi Arabia ilisema imewafuta kazi maafisa wawili wa ngazi ya juu katika serikali ya Mohammed bin Salman, ambao ni Naibu mkuu wa idara ya ujasusi jenerali Ahmed al Assiri na mshauri wa habari Saud Qahtani.

Qahtani amepigwa marufuku ya kusafiri na kwa sasa anachunguzwa japo hakuna maelezo yoyote yaliotolewa juu ya hatma ya jenerali Assiri.

Marekani itawawajibisha wahusika wote wa mauaji ya Jamal Khashoggi

Kulingana na bwana Hellyer anaefanya kazi katika taasisi ya mambo ya kifalme mjini London, hii ni njia moja ya serikali ya Saudi Arabia kujikosha lakini bado suali litabakia pale plae la ni nani hasaa alietoa amri ya kuuwawa kwa mwanahabari Jamal Khashoggi.

Saudi Arabien Treffen US-Aussenminister Pompeo und dem Kronprinz Mohammed bin Salman
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo na mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: picture-alliance/dpa/SPA

Wakati huo huo Uturuki imepongeza hatua iliochukuliwa ya hukumu ya kifo kwa wahusika wa mauaji ya mwanahabari huyo lakini ikasema hatua zilizochukuliwa hazitoshi. Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mevlut Cavusoglu amesema Uturuki ingelipenda wote watakaohusika na muaji hayo washitakiwe Uturuki.

Tangazo hilo linatolewa wakati jamii ya  kimataifa ikiendelea kupaza sauti juu ya mauaji ya Jamal Khashoggi aliyekuwa na umri wa miaka 59 ambaye alionekana mara ya mwisho tarehe 2 Oktoba, katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul akitafuta nyaraka za kumuwezesha kufunga ndoa na mmpenzi wake raia wa Uturuki.

Siku ya Jumapili waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alizungumza na Mohammed bin Salman kwa njia ya simu na kumfahamisha kuwa Marekani itawawajibisha wote watakaohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi.

Mwandishi: Amina Abubakar AFP/Reuters/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga