Saudi Arabia, Umoja wa Mataifa waitisha mkutano wa ufadhili kwa Yemen | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

YEMEN

Saudi Arabia, Umoja wa Mataifa waitisha mkutano wa ufadhili kwa Yemen

Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia zimeshirikiana kuitisha mkutano wa wafadhili kwa njia ya mtandao wakidhamiria kukusanya zaidi ya dola bilioni 2 kuisaidia Yemen, taifa lililokumbwa na ufukara, mauaji, na sasa COVID-19.

Ukienda kwenye soko kuu la Sanaa, unakutana na nguo za kila rangi, vitabu vikongwe, tani kwa tani za peremende, na pirika za ngia-toka kama kwamba hakuna kinachoendelea.

Watu hapa wanabanana kwenye mitaa myembaba, wakisimama karibu sana na washitiri, wakipatana bei za bidhaa. Si rahisi hapa kuweka  masafa ya mita moja na nusu baina ya mtu na mtu.

"Bila shaka, tunaogopa. Lakini nalazimika kutoka kununuwa mahitaji ya wanangu. Naogopa lakini sina budi kuja kununuwa mahitaji muhimu. Tunatarajia dunia inatuona na inafahamu kuwa sisi Wayemeni tupo mitaani lakini pia tunaogopa virusi vya korona vinavyouwa," anasema Qaboos Bin Said Al Houkaly, mmoja ya wale wachache waliovaa barakowa kwenye soko hili.

Mwanzoni mwa mwezi Aprili, mtu wa kwanza aligundulika na virusi vya korona nchini Yemen na tangu hapo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa kwamba idadi ya walioambukizwa inapanda, katika nchi ambayo tayari mamilioni wanatapatapa angalau waweze kuishi siku yao moja.

Hata kabla ya korona, Yemen ilishakuwa taabani

Jemen | Corona Händehygiene in Slums

Hata bila COVID-19, Yemen ilishasambaratishwa kwa vita na ufukara.

Kumekuwa na vita kati ya Wahouthi, kabila la watu wa kaskazini mwa nchi hiyo, na Saudi Arabia, ambayo inaunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa lakini isiyo na nguvu. Huu ni mwaka wa tano sasa.

Zaidi ya watu 100,000 wameshauawa, milioni kumi sasa wako hatarini kufa njaa. Hata kama kusingelikuwa na janga la COVID-19, hali ilishakuwa mbaya tayari.

"Mara nyingi inakuwa vigumu kwetu kuyafikia maeneo mengine na kusambaza maji na chakula kwa usalama, kwa sababu ya mapigano na mashambulizi ya anga. Pia tunalazimika kupata vibali vya kuyafikia maeneo hayo na wakati mwengine hutukatalia kwa sababu mbalimbali. Hizi zilikuwa changamoto kubwa kabla ya COVID-19 na bado zinaendelea hadi sasa," anasema Aaron Brent, mkurugenzi wa shirika la misaada la CARE nchini Yemen.

Ukiacha hayo, kuna tatizo la mfumo mbovu wa afya. Watu wengi ni wagonjwa ama majeruhi, lakini hawawezi kugharamikia matibabu yao.

Hata fedha ya kumsafirisha mtu kumpeleka kituo cha afya, ambayo mara nyingi ni masafa marefu kutoka maeneo ya milimani, hubidi kuchangiwa na watu kadhaa. Shirika la CARE linakisia kuwa kiasi cha watu 30,000 wamekufa kipindi hiki cha vita kwa sababu hawakuweza kutibiwa nje ya nchi.

Mkutano wa leo unaoitishwa kwa njia ya mtandao kwa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Saudi Arabia unadhamiria kukusanya kiasi cha dola bilioni 2.4, katika wakati ambapo mashirika ya kibinaadamu yanayotowa huduma zake nchini Yemen yakikabiliwa na uhaba mkubwa kabisa wa fedha ilhali taifa hilo fukara zaidi kwenye ulimwengu wa Kiarabu likikabiliwa na vita na janga la korona.

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanasema hadi sasa yameshalazimika kufunga takribani ya asilimia 75 ya shughuli zao nchini Yemen.